August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa aongoza mazishi ya Askofu Isuja

Spread the love
KASIMU Majaliwa, Waziri Mkuu amewaongoza maelfu ya waumini wa Kanisa Kathoriki Jimbo Kuu la Dodoma wakati wa mazishi ya Mathias Isuja, aliyekuwa askofu mstaafu wa jimbo hilo, anaandika Dany Tibason.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano imepokea kifo hicho kwa masikitiko kutokana na juhudi za kimaendeleo alizokuwa akizifanya askofu Isuja enzi za uhai wake.
Amesema, kutokana na kazi za Askofu Isuja, serikali imeahidi kuhakikisha inaenzi kazi zake ambazo zilionekana kuwa na tija kwa taifa likiwemo suala la kukuza elimu nchini.
“Marehemu askofu ametutoka wakati ambao bado tulikuwa tunamuhitaji,amefanya kazi nzuri sana za kikanisa pamoja na za kijamii ambazo sisi kama serikali hatuna budi kuzienzi na kuziendeleza,” amesema.
Mbali na hilo, amewataka wote nchini kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi badala ya kufanya kazi kwa lengo la kujinufaisha wenyewe.
Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania amesema, askofu Isuja ni kati ya viongozi ambao walifanya kazi katika mkoa wa Dodoma katika mazingira magumu zaidi.
Ameeleza kwamba, kufanya kazi katika mazingira magumu kulitokana na hali halisi ya mkoa wa Dodoma kutokana na jinsi mungu alivyouwezesha kuwa.
“Dodoma ni kati ya mikoa yenye watu masikini na hiyo inatokana na hali ya Mungu alivyoiweka, lakini hivi karibuni nilisikia kauli ya kiongozi mmoja ambaye aliwabeza wakazi wa mkoa wa Dodoma na kuwaita watu wenye udumavu wa akili.
“Hivyo inaonekana kuwa watu wa Dodoma hawana akili na wamedumaa, kauli ya aina hiyo inawafanya wakazi wa Dodoma kukata tamaa na siyo kauli nzuri kwa kutolewa na kiongozi mkuu bali alitakiwa kuwatia moyo na kuona jinsi Mkoa wa Dodoma ulivyo na si vinginevyo,” amesema Ndugai.
Kauli hiyo ya Ndugai ilimlenga Chiku Ghallawa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ndiye aliwahi kusema asilimia 60 ya wakazi wa Dodoma wamedumaa akili.
Beatus Kinyahiya, Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katholiki la Dodoma amewataka waumini wote kumuiga kimatendo marehemu askofu Isuja kwa kutenda mema na kimaendeleo.
Amesema wakati wa uhai wa Isuja alifanya maandalizi yake mwenyewe kwa kujishonea nguo ambazo alizifanya kuwa maandalizi ya kumzika nazo wakati wa kifo chake.
“Marehemu Isuja alikuwa haogopi kifo na ndiyo maana aliweza kuwa na ujasili wa kujishonea nguo kwa ajili ya maandalizi ya kumvisha wakati wa kifo chake, pia aliagiza azikwe ndani ya kanisa kuu la Paul Msalaba jambo ambalo viongozi na waumini wanatakiwa kuliiga”alieleza.
Wengine waliohudhuria ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda; Spika Mstaafu, Anne Makinda; mawaziri, wabunge, Mke wa Edward Lowassa (Regina Lowassa) pamoja na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini.
error: Content is protected !!