December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa amtaka bosi Tanesco kusimamia ipasavyo JNHPP 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, (watatu kushoto) akikagua hatua za utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Tito Mwinuka kusimamia mradi ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115 ukamilike kwa wakati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Rufiji … (endelea)

Vilevile, Waziri Mkuu amemwagiza mkandarasi anayejenga mradi huo aukamilishe kwa wakati kwa sababu imebainika  mvua zinazoendelea kunyesha nchini haziathiri utekelezaji wa ujenzi huo.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana Alhamisi tarehe 14 Mei 2020 akiwa katika ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo. Amesema ameridhishwa maedeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.

“Nimetembelea eneo la mradi na kujionea shughuli zote zinazoendelea, kazi inayofanyika ni ya uhakika huku kukiwa na matumaini makubwa ya kukamilisha mradi mapema kabla ya muda uliopangwa,” alisema

Mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unajengwa na kampuni ya Arab Construction kwa pamoja na kampuni ya Elsewedy Electric zote za kutoka nchini Misri.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye grid ya Taifa na kuifanya nchi kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika ukaguzi wa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)

Mbali na kuliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, pia mradi huo umewezesha kupungua kwa changamoto ya ajira baada ya Watanzania wengi wakiwemo wakandarasi kupata ajira za kudumu na za muda mfupi.

Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitakachosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa.

Hafla ya utiaji saini ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi ilifanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Desemba, 2018 na kushuhudiwa na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly.

Mradi huo ni njia sahihi ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

error: Content is protected !!