August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa ammwagia manoti aliyekuwa mraibu dawa za kulevya

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa kiasi cha Sh milioni tano kwa Amina Mshana aliyekuwa mraibu wa dawa za kulevya kwa muda wa miaka 12 ili atumie fedha hizo kuratibu mwenendo wa masomo ya mwanaye.

Pia ametoa wito kwa Watanzania kuwafichua wafanyabiashara, wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo tarehe 2 Julai, 2022 katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupambana na dawa za kulevya duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.

Awali akitoa ushuhuda katika maadhimisho hayo, Amina amesema katika muda wa miaka 12 aliokuwa akitumia dawa za kulevya, amekumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo kulazimika kushiriki biashara haramu ya uchangudoa ilia pate fedha za kuvuta unga.

Pia alipata ujauzito ambao ulipata athari na kulazimisha kujifungua ukiwa na miezi sita na mtoto huyo mchanga kukaa kwenye chupa miezi tisa.

Amefafanua kuwa mwanaye huyo ambaye sasa yupo darasa la kwanza, ndiye mwanafunzi kinara darasani.

Aidha, akihutubia washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri Mkuu amesema kutokana na ushuhuda wa dada Amina, jambo kubwa ambalo watanzania wamejifunza ni yeye kushiriki kikamilifu kumlea mtoto yule huku mzazi wake akiondoa uwepo wa dawa mwilini mwake.

“Tumemuona mtoto akiwa na afya njema, ameanza shule na sasa yupo darasa la kwanza, tena anakuwa wa kwanza darasani.

Kwa kuwa taasisi ipo ndani ya ofisi ya waziri mkuu, nataka tumuunge mkono dada huyu kumtunza mtoto wake ambaye leo anafanya vizuri darasani.

“Ofisi yangu itampa milioni tano, itakayomsaidia kuratibu mwenendo wa masomo ya mtoto huyu, kwa kuwa elimu ya msingi mpaka kidato cha sita Rais Samia amesema masomo hayo yatapatikana bure, lakini mtoto huyu ana mahitaji mengine kama vile sare madaftari, viatu, chakula chake.

“Dada muone msaidizi wangu ili uone utaratibu wa kupata milioni tano, itakayokusaidia kumlea mtoto huyu mpaka amalize darasa la saba afaulu aende sekondari, tunamuombea aendelee kuwa wa kwanza hadi afike chuo kikuu,” amesema.

Aidha, amesema dawa za kulevya zina athari kubwa, hivyo vijana wanaotumia waache mara moja lakini wale wanaofikiria kutumia wasijiingize kwenye janga hilo.

Amesema ukamataji wa mkupuo wa dawa za kulevya nchini umeongezeka jambo ambalo si dalili nzuri hivyo ni muhimu Watanzania wakaungana kupambana na waingizaji wa dawa hizo nchini.

“Matukio ya ukamataji kwa mkupuo yameongezeka tangu kuteuliwa kuwa Kamishna Jenerali, (Gerald Kusaya) mfano Aprili mwaka 2021 zilikamatwa kilo 855 zikijumuisha kilo 504.36 za heroin na 335 za methamphetamine, Juni 2021 zilikamatwa kilo 57.3 za heroin na kilo 73.6 za methamphetamine, Aprili 2022 jumla ya kilo 174 za heroin.

“Hii sio dalili nzuri, ni muhimu Watanzania tukaungana pamoja kupambana na hawa waingizaji wa dawa hizi nchini,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kukemea usafirishaji wa dawa za kulevya na matumizi yake.

Pia viongozi wa dini wanalo jukumu kwa jamii kukemea matumizi haramu ya dawa za kulevya.

“Tatu, wana habari endeleeni kutumia vyombo vyenu na kalamu yenu kukemea kwa nguvu zote biashata na matumizi ya dawa za kulevya, toenu habari kwa umma kuhuduma zinazotolewa kwenye maeneo ya matibabu wa dawa za kulevya.

Lengo letu ni kuhakikisha nguvu kazi ya taifa inalindwa na kuendelezwa,” amesema.

Awali Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya amesema kauli mbiu katika maadhimisho inasema, “Tukabiliane na changamoto za dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii”.

Amesema kauli mbiu hiyo inakumbusha kuwa dawa za kulevya ni tatizo linaloathiri maendeleo ya jamii hivyo wanatakiwa kushirikiana katika kudhibiti changamoto zinazotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2017 hadi Juni 2022, jitihada zimefanyika kudhibiti dawa za kulevya zinazolishwa nchini ambazo ni bangi na mirungi zinazolishwa nchini,

“Katika kipindi miaka mitano kuanzia 2017, jumla ya tani 134.67 za bangi na tani 100 za mirungi, zilikamatwa wakati zikisafirishwa au kuuzwa maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Amesema wamefanikiwa kusambaratisha mtandao uliokuwa unafanya biashara za mirungi kwenda nchini Ethiopia kwa njia ya vifurushi huku wahalifu wakijinasibu kusafirisha dawa za tiba mbadala.

“Operesheni zilizofanyika katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi hasa mikoa ya Arusha, Mara, Morogoro, Kagera, Ruvuma na Pwani zilifanikisha uteketezaji wa hekari 715.7 za bangi aidha hekari 64.5 za mirungi maeneo ya Same mkoani Kilimanjro.

“Katika dawa za kulevya za viwandani, kilo 1906 za heroin zilikamatwa katika kipindi cha miaka mitano, kiasi hicho ni mara mbili zaidi ya kilichokamatwa katika miaka mitano ya nyuma na ni kiasi kikubwa kuwahi kufikishwa tangu nchi yetu ipate uhuru,” amesema.

error: Content is protected !!