Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, Serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa korona (UVIKO- 19) kwa kuanzisha rasmi utekelezaji wa afua ya chanjo na kuratibu upatikanaji wa chanjo hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Amesema hadi tarehe 28 Februari, 2022, jumla ya dozi 9,845,774 zimepokelewa nchini, dozi 5,426,840 sawa na asilimia 55 zimesambazwa mikoani na watu 2,664,373 walichanjwa dozi kamili.

“Nitoe wito kwa Watanzania wote kuendelea kupata chanjo hizo ambazo ni za bure na zinapatikana katika maeneo yote nchini,” amesema

Majaliwa amesema hayo leo Jumatano, tarehe 6 Aprili 2022 bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka 2022/23 ya Sh.148.89 bilioni na Sh.132.7 bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Amesema katika kupunguza athari za UVIKO -19 nchini, Serikali ilipatiwa mkopo wa Sh.1.3 trilioni na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

Majaliwa amesema, sekta zilizonufaika na Mpango huo ni maji (shilingi bilioni 139.4), elimu (shilingi bilioni 368.9), afya (shilingi bilioni 466.9), utalii (shilingi bilioni 90.2), jamii inayoishi kwenye mazingira magumu (shilingi bilioni 5.5), na kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu (shilingi bilioni 5).

Aidha, shilingi bilioni 231 zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 5 kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo uratibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *