October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa aendelea kung’ata watumishi, amsimamisha mwingine

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Omary Chingwile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Liwale na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

“Hatuwezi kufanya mchezo na fedha ya Serikali. Tunahitaji kila mradi uende vizuri, fedha iliyoletwa lazima itumike kama ilivyokusudiwa,” amesema Majaliwa

Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza matumizi mazuri ya fedha za umma ili zikamilishe miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote anayetumia vibaya fedha za umma.

Waziri Mkuu amemsimamisha kazi mtumishi huyo jana Alhamisi, tarehe 7 Oktoba 2021, wakati akizungumza na madiwani, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi.

Pia, Majaliwa amelitaka Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Liwale lisimamie vyema fedha za miradi zinazotolewa katika Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

“Waheshimiwa madiwani, Halmashauri yenu inakusanya mapato hadi asilimia 100 lakini hatujawahi kuona mradi wowote unaotekelezwa na halmashauri na ukawa wa mfano.”

Alisema Halmashauri hiyo imekuwa ikiweka makadirio madogo ya makusanyo ili ionekane inakusanya kwa asilimia kubwa lakini hata mapato yanayokusanywa, hayakusanywi kwa njia za kielektroniki na kumuagiza Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Gervas Bidogo kuhakikisha vifaa vyote vya kukusanyia fedha kwa njia ya kielektroniki (POS) vinafanya kazi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli kufuatilia fedha za wakulima wa korosho na ufuta ambao hawajalipwa na vyama vya ushirika abavyo vilikusanya mazao yao.

“Nakupongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi Afisa Ushirika Bw. Ephraim Kipomela kutokana na upotevu wa fedha za ushirika usiishie hapo hakikisha vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinafanya uchunguzi na kubaini namna fedha hizo zilivyopotea,” alisema na kuongeza

“Afisa Kilimo wa Wilaya ya Liwale wahamasishe wakulima kutumia mbegu mpya za korosho ambazo zinazalisha matunda mengi na kwa muda mfupi, ongeza pia uhamasishaji kwenye kilimo cha mazao ya chakula kwa sababu Mheshimiwa Rais amepunguza tozo na gharama kwenye pembejeo na sasa wakulima wa korosho wanapata mbolea ya salfa bure.”

Awali, akikagua ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Magereza, Waziri Mkuu amempongeza Mkuu wa Magereza wa Liwale, Gilbart Sindani kwa ubunifu wa kuanzisha mradi wa uuzaji wa mbao jambo lililowezesha gereza hilo kujiendesha na kujenga majengo mapya ya utawala pamoja na nyumba za wafanyakazi.

Huyu ni mtumishi wa nne kusimamishwa mkoani humo akitanguliwa na maafisa mapato watatu wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoani humo kusimamishwa. Waliosimamishwa ni Bahaye Shilungushella, Ally Kijonjo na Mohamed Samodu.

Pia, Majaliwa aliagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) pamoja na Jeshi la Polisi wawachunguze na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

error: Content is protected !!