May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa abanwa bungeni fedha za miradi kurudi hazina

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amebanwa bungeni kuhusu utaratibu wa fedha za miradi zinazochoelewa kutumika, kurudishwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina wa Wizara ya Fedha na Mipango. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).

Leo Jumatano tarehe 3 Juni 2021, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, bungeni jijini Dodoma, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, alimhoji Waziri Majaliwa, akisema Serikali haioni umuhimu wa kusitisha mpango huo.

Kingu alisema kuwa, utaratibu huo wa fedha za miradi ya maendeleo kurudishwa hazina, unaathiri maendeleo ya wananchi, huku akilalamikia hatua ya Serikali kuchelewa kupeleka fedha hizo, kisha kuzitwaa baada ya mwaka wa fedha husika kukoma.

“Sasa hivi pamekuwa na utaratibu ambao Serikali inapelekea fedha za maendeleo kwenye halmashauri, hasa kuanzia Machi, Aprili na Mei. Fedha hizi zinapokuwa hazijatumika, mwaka wa fedha unapoisha, zinarudishwa hazina na kuathiri utekelezaji miradi ya maendeleo ya wananchi,” amesema Kingu.

Kingu amesema “Ninatoa mfano wa majimbo mengi Tanzania, tumepokea fedha za ujenzi wa miradi, lakini zimepokelewa mwezi wa Aprili hadi Mei, ni wazi itakapofika mwisho wa mwaka wa fedha, zitakuwa hazijatumika, zitarudi hazina na hatujui zitakwenda kutumika namna gani.”

“Je, Serikali haioni umuhimu wa kusitisha mpango huu na kuruhusu fedha hizi, ambazo tayari zinagusa wananchi wanyonge zisirudi hazina, badala yake kuwe na utaratibu wa kuzitumia?” amesema Kingu.

Akijibu swali hilo, Waziri Majaliwa amesema, Wizara ya Fedha na Mipango imeagizwa kurekebisha kanuni hizo, ili kuweka utaratibu utakaoruhusu fedha za miradi kutumika baada ya mwaka wa fedha kuisha.

“Niliwaagiza wizara ya fedha kubadilisha utaratibu, kufanya maboresho kwenye kanuni zetu, kuweka kanuni ambayo itaruhusu miezi kadhaa baada ya mwaka wa fedha wa bajeti kuisha, ili fedha zile ziweze kukamilisha kazi,” amesema Waziri Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Majaliwa amesema Serikali itawabana watendaji watakaoshindwa kutumia fedha hizo kwa makusudi, kwa kigezo cha kutegemea kupewa muda wa ziada.

Elibariki Kingu, bungee wa Singida Maghalibi (Ccm)

“Ingawa kwenye hili hatutahitaji mwanya wa wazembe, kukaa na fedha bila kuzitumia, akitegemea ataongezewa muda. Pamoja na kanuni tunayoboresha, tutaweka kipengele cha kumbana mtendaji kuhakikisha fedha inapoingia itumike kwa muda uliopangiwa,” amesema Waziri Majaliwa.

Aidha, Waziri Majaliwa amesema, utaratibu huo uliwekwa ili kuhakikisha watendaji wanatekeleza miradi kwa muda uliopangwa.

“Ni kweli tuliweka sheria ambazo zinataka fedha zinapofika angalau tarehe 15 Juni ya mwaka wa mwisho wa fedha, kama halmashauri haijamudu kufanya matumizi lazima zirudi ,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza:

“Na tuliweka utaratibu kama halmashauri imepelekewa fedha na wamefika muda wa mwisho kushika fedha na kutaka kuzirudisha , waandike barua kuonesha mpaka tarehe hii tuna fedha ambazo hazijafanyika kwa sababu ya taratibu za manunuzi.”

error: Content is protected !!