January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaji wa3 kusikiliza kesi ya mitandao

Spread the love

JOPO la Majaji watatu leo limeanza rasmi kusikiliza shauri linalohusu kupinga Sheria ya Makosa ya Mitandaoni, Na. 14 ya mwaka 2015. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Prof. John Eudes Ruhangisa, mwenyekiti wa majaji hao, anashirikiana na Jaji Winfrida Koroso na Jaji Lugano Mwandambo kusikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa na wakili wa kujitegemea wa jijini Dar es Salaam, akiungwa mkono na asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu nchini.

Leo kesi hiyo imetajwa mbele ya mfungua shauri hilo, Jebra Kambole ambaye anashirikiana na mawakili Benedict Ishabakaki anayefanya kazi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDs). Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mlalamikiwa, aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Richard Kilanga.

Mawakili wengine wanaoshiriki kufuatilia shauri hilo lililosajiliwa kwa Civ. Case, Na. 32/2015, pamoja na Kambole, ni John Seka, Massawe Fulgence, Harold Sungusia, Boka Iyamuya, Neema Ndemno na Geremia Mtobesia.

Jaji Prof. Ruhangisa amesema kwa mujibu wa sheria, baada ya kutaja shauri, jopo linaelekeza upande wa mlalamikiwa, Serikali, uwasilishe majibu ya madai katika shauri ndani ya siku 14 kuanzia shauri lilipofunguliwa jalada Mahakama Kuu, ambayo ni jana.

Maelekezo mengine ni juu ya mlalamikaji, wakili Kambole, kuwasilisha majibu ya hoja za mlalamikiwa, ndani ya siku saba.

Jaji Ruhangisa amesema baada ya hatua hizo kukamilika, wawakilishi wa pande hizo mbili watatakiwa kufika mbele ya jopo la majaji hao Oktoba 22, mwaka huu kwa ajili ya usikilizaji wa shauri. Alihimiza shauri litaitwa saa 7 mchana.

Wakili Kambole alipotoka nje ya jengo la Mahakama Kuu, alikutana na waandishi wa habari na kueleza kuridhishwa kwake na hatua za awali za shauri hilo, pamoja na matumaini yake kuwa “anaimani haki itatendeka na Watanzania watapata haki zao zinazofiywa na sheria hiyo.”

Wakili huyo alisihi wananchi watulie na kuendelea kumpa ushirikiano wa karibu kuhusu shauri ambalo amesema yeye amechukua hatua ya kuwakilisha maoni ya mamilioni ya Watanzania kwa kuwa ndivyo sheria inavyoelekeza.

“Nimeamua kuianzisha kwa manufaa ya wananchi wote ili tuweze kupata haki zetu. Na ikishindikana hapa, basi tutasonga mbele katika Mahakama ya Afrika Mashariki hadi tupate muafaka,” amesema.

Katika shauri hilo, Kambole anapinga vipengele kadhaa vya sheria husika kwa maelezo kwamba vinavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Vipengele vinavyopingwa ni kifungu cha 4, 5 na 45 (4) cha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ambavyo vinazuia haki ya kupata na kutoa taarifa, na Ibara ya 18 ya Katiba.

Vingine ni vifungu 6, 7, 8, 10, 11, 14, 19, 21 na 22 anavyoona vina maneno yasiyo na tafsiri, hivyo kuweza kusababisha tafsiri mbaya kwa watekeleza sheria na matokeo kuweza kuwa ya kuvunja haki za binadamu, kinyume na Ibara ya 17 ya Katiba.

Vifungu 31,33,34,35 na 37 vya sheria hiyo vinatoa mamlaka kwa Polisi kufanya upekuzi bila ya idhini ya Mahakama hivyo ni uvunjufu wa haki za binadamu na inakinzana na Ibara ya 16 ya Katiba.

Vipengele vingine, Kifungu cha 38 cha sheria hiyo kinanyima haki ya mtu kusikilizwa na Mahakama huvyo inakinzana na Ibara ya 13 (6) ya Katiba pamoja na kifungu cha 47 (1) cha sheria hiyo kinanyima Polisi kufanya kazi zao kama ilivyo katika Sheria hii.

error: Content is protected !!