January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maimu wa NIDA matatani

Spread the love

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu anachunguzwa utendaji wake baada ya kusimamishwa kazi rasmi kuanzia leo. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Maimu aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2006 mara baada ya kuingia madarakani kwa Rais Jakaya Kikwete, aliyekuja na mradi wa kutoa vitambulisho vya taifa kwa wananchi na wageni.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Maimu wa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, na akamsimamisha kazi kwa lengo la kuruhusu kufanywa kwa uchunguzi wa manunuzi ya bidhaa na huduma ndani ya mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli ameagiza kufanyike uchunguzi wa namna tatu: (1) kujua namna mamlaka hiyo ilivyopata huduma mbalimbali kupitia utaratibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, 2004. Uchunguzi huu imetakiwa ufanywe na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).

(2) Uchunguzi wa pili ni utakaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – Controller and Auditor General (CAG) – kwa ajili ya kujua kiwango hasa cha manunuzi ya huduma kwa dhana ya thamani halisi ya kifedha ya bidhaa na huduma zilizonunuliwa kitaalamu ikiitwa Value for Money.

(3) Uchunguzi wa tatu ni ule utakaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa ajili ya kuangalia kama kulikuwa na vitendo vya rushwa wakati wa manunuzi.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imesema Rais Magufuli amepata taarifa kuwa NIDA imetumia Sh. 179.6 bilioni kuandaa vitambulisho ambavyo inaonekana kasi ya upatikanaji wake ni ndogo.

Katika uchunguzi utakaofanywa, Ikulu imesema mbali na Maimu, wengine watakaochunguzwa ni waliokuwa wasaidizi wake katika idara ya Teklonojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Joseph Makani; idara ya Ugavi, Rahel Mapande ambaye ni Afisa Ugavi Mkuu; idara ya Sheria, Sabrina Nyoni ambaye ni Mkurugenzi na idara ya Usafirishaji, George Ntalima ambaye ni Afisa Usafirishaji.

Hatua ya Rais Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, 2015, imegusa eneo ambalo lilipata kulalamikiwa matumizi yake hasa kwa kuonekana mradi wenyewe kama haukuanza kutekelezwa katika njia za uwazi.

Hata hivyo, menejimenti ya NIDA iliwahi kulalamika kwamba shughuli zake za utoaji wa vitambulisho zilizorota na kuathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na kutopatiwa fedha zilizokuwa zimepangwa.

Zipo taarifa kuwa sehemu kubwa ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mamlaka hiyo, zilichotwa na Serikali Kuu na kupelekwa kugharamia shughuli za upitishaji wa Rasimu ya Katiba mpya, chini ya Bunge Maalum la Katiba.

error: Content is protected !!