Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mahojiano Rais Samia, BBC yaibua mvutano kesi ya Mbowe
Habari za SiasaTangulizi

Mahojiano Rais Samia, BBC yaibua mvutano kesi ya Mbowe

Spread the love

 

MAHOJIANO aliyoyafanya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kugusia kesi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, yamebiliwa mahakamani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ni mahojiano yaliyofanyika Jumatatu ya tarehe 9 Agosti 2021, ambapo kwenye mahojiano hayo maalum, Rais Samia aliulizwa kuhusu mashtaka dhidi ya Mbowe kama yamefunguliwa kwa mlengo wa kisiasa.

Leo Jumanne, tarehe 26 Oktoba 2021, mbele ya Jaji Joackim Tiganga anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu, mahojiano hayo yameibuliwa wakati shahidi wa Jamhuri, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai akitoa ushahidi wake.

RPC Kingai alikuwa akijibu maswali ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala hali iliyomfanya Jaji Tiganga kuzuia kuulizwa maswali hayo kwani shahidi huyo hajafika kutoa ushahidi kama muhimili.

Mahojiano ya Wakili Kibatala na majibu ya RPC Kingai yalikuwa hivi;

Wakili Kibatala: Unafahamu Detention Register ili iwe Genuine Unatakiwa ionekane vipi nje na Ndani

Shahidi RPC Kingai: Hapana sifahamu

Kibatala: Kwanini ufahamu na wewe ni Afisa wa Polisi kwa muda wa miaka 18

Shahid: Kuna maswali unataka kunibana na mimi nakwepa

Wakili Kibatala: Kabla ya kumkamata Mbowe katika Kongamano la Katiba Mwanza, mlikuwa mnajua kuwa Mbowe anasafiri nje ya nchi

Shahidi RPC Kingai: Ndiyo tulikuwa tunajua

Kibatala: Wewe mtu Mzima inaingia akilini mtu ana kesi ya ugaidi mnampeleleza mkamruhusu asafiri mpaka arudi mwenyewe

Shahidi: Ndiyo. Inawezekana. Tulikuwa tuna mpelelezi ndani na nje ya nchi.

Wakili Kibatala: Ulishawahi kuitaarifu mamlaka zingine nje ya nchi kuwa anayekuja ni gaidi?

Shahidi RPC Kingai: Hapana. Hakuwa Flight Risk.

Kibatala: Umesikiliza mahojiano ya BBC na Rais Samia?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili wa Serikali: Objection! Mheshimiwa Jaji naomba tuangalie sheria kama zinaruhusu au kutubana.

Wakili wa Pili wa Serikali: Majibu anayotaka ni kuhusu mahojiano. Aulizwe maswali ambayo yeye yanamhusu.

Jaji: Peter (Kibatala) kwa hoja hizo. Unasemaje?

Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji samahani sana. Tulifungua kesi ya kikatiba namba 21 ya mwaka 2021. Walalamikiwa walikuwa DPP na Mwanasheria Mkuu. Jaji Mgeta akasema hivi: Mahakama yake inafungwa haiwezi kuingilia kesi hiyo, na kama kuna hoja anaomba ziwasilishwe katika kesi ya jinai inayoendelea Katika Mahakama Kuu.

Jaji Tiganga: Sasa huyu amekuja kama Executive Order au kama shahidi?

Wakili Kibatala: Ikumbukwe Mahakama ipo majaribuni pia kwamba sasa Rais ameshasema.

Jaji: Naona shahidi unam-treat kama shahidi anayekuja kuwakilisha muhimili, wakati tumemuapisha kuja kutoa ushahidi kwenye jambo alilolifanya

Wakili Kibatala: Kama hutojali umauzi ule tumekatia Rufaa, mimi ukiniambia hapa siyo mahali pake nilitumia hiyo Statement

Jaji Tiganga: Mengine yote unaweza kumuuliza, lakini tusimuilize swali ambalo kasema mtu mwingine.

Kibatala: Nauliza kama forum hapa ikifungwa tukienda kwingine wasiseme hatukuileta hapa. Hatuwezi kusema kwa hii trial mlango pia umefungwa.

Jaji: Nafahamu mna mashahidi mnaweza kuwaleta kuwahoji kauli hizo.

Katika mahojiano hayo, Rais Samia alisema mahakama hiyo ndiyo itakayothibitisha kama Mbowe ana hatia au hana hatia.

“Kwa sababu jambo liko mahakamani, sina uhuru wa kulizungumzia kwa sana, nadhani tuiachie mahakama ionyeshe ulimwengu hizo shutuma walizomshutumu ni za kweli, au si za kweli. Mahakama itaamua,” alisema Rais Samia

Alipoulizwa kama Mbowe ameshtakiwa kwa makosa hayo kwa sababu za kisiasa, Rais Samia alijibu “mimi sidhani kama yamechochewa kisiasa, kwa sababu ninavyojua Mbowe alifunguliwa kesi Septemba 2020, yeye pamoja na wengine na kama ulivyosema mashtaka ya ugaidi na kuhujumu uchumi.”

“Nadhani wengine kesi zao zimesikilizwa, wengine wamepewa hukumu zao wanatumikia. Yeye upelelezi ulikuwa haujaisha, uchunguzi ulikuwa unaendelea. Kwa hiyo amekwenda tumeingia kwenye uchaguzi,” alisema Amri Jeshi hiyo mkuu

“Amemaliza uchaguzi, nadhani sasa Polisi wamekamilisha uchunguzi wao, wamemhitaji waendele na kazi yao,” amesema Rais Samia.

Alisema kilichomchelewesha Mbowe kutounganishwa na wenzake katika kesi hiyo ni mwanaasiasa huyo kuwa nje ya nchi.

“Kama utakumbuka Mbowe kipindi kirefu hakuwepo nchini, alikuwepo Nairobi. Kwa nini kakimbia sijui, lakini alivyoingia tu nchini kaitisha maandamano ya madai ya katiba, nadhani ni mahesabu amejua kwamba ana kesi ya aina hiyo na hii vurugu akikamatwa aseme kwa sababu ya katiba,” alisema Rais Samia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!