July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahangaiko ya maji yanazusha vifo Ilota

Wakazi wa kijiji cha Ilota, Mbeya wakitoka kuchota maji kwenye makonongo

Spread the love

WAKAZI wa kijiji cha Ilota, Kata ya Mshewe, mkoani Mbeya wanatembea umbali mrefu, wanapoteza muda mwingi, wanapata ulemavu.

Wengine hufa kutokana na kusaka maji katika mazingira hatarishi, MwanaHALISI online linaeleza.

Baada ya kero hizo kuibuliwa wakati wa kampeni ya uraghibishi iliyofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwenye Kata ya Mshewe Mei 2013, kulifanywa uchunguzi na kubainika maji wanayotumia wakazi baada ya kuyapata kwa mateso katika mashimo ya Asante, Isanyanto na Ibogonyo, yamepimwa na vipimo kuonesha “hayafai kwa matumizi ya binadamu.”

Mwenyekiti wa kitongoji cha Ilota A, Dickson Elias alisema mwaka 2007 watu wanne walikufa katika kijiji hicho kutokana na kunywa maji hayo.”

Anasema, “Watu hao walikufa kwa kuugua kipindupindu baada ya kunywa maji haya, na mmoja kati ya marehemu hao alikuwa mkazi wa kitongoji changu.” Anamtaja mkazi wake huyo kuwa ni Hasara Mwasheto.

Mkazi mwingine, Ester Boazi, alisema ili kuyapata maji hayo, wanalazimika kushuka na kupanda juu ya miamba yenye mteremko mkali ambako hufukuzwa na nyoka aina ya chatu, hali inayosababisha ajali nyingi na mara kadhaa vifo.

“Mwaka 1996 mzee aliyeitwa Mwangolombe, aliyekuwa akiishi peke yake, alifariki baada ya kuteleza na kudondoka kwenye korongo hili wakati akitafuta maji. Aling’oka meno yote. Maiti yake ilikuwa ikivuja damu.Tulipata shida sana kuitoa na kuipandisha juu,” alieleza Ester.

Ester alisema kutokana na shida ya maji, shule haina walimu wa kike. Wapo wa kiume na wanaishi umbali wa zaidi ya kilometa 10, hali inayosababisha wanafunzi wa kike kushindwa kueleza matatizo yao ya kijinsia kwa walimu wa kiume.

Ukosefu wa usafiri hapo, unazusha tatizo la uchelewaji wanafunzi shuleni. Hufika waki wamechoka na hulazimika kuwaagiza wanafunzi kwenda kutafuta maji kwenye mashimo kwa ajili ya matumizi ya shule.

“Mwaka 2004 wanafunzi walikwenda kwenye korongo kutafuta maji. Wakakimbizwa na chatu, wakateleza, wakadondoka. Mmoja aling’oka meno hadi leo anaishi na mapengo, mwingine alichanika mdomo na watatu alivunjika mkono,” anasema.

Sophia Damson, mkazi wa kitongoji cha Mpona B, kijiji cha Ilota, anasema wajawazito hawajasalimika na kadhia hiyo. Wanalazimika nao kuhangaikia maji kama kinamama wengine. Zipo kesi za wajawazito kujifungulia wakiwa ndani ya mahangaiko hayo kutokana na kutumia nguvu kubwa kupanda miamba huku wamebeba ndoo za maji kichwani.

“Uchungu huwashika na kujifungua kabla ya muda,” anasema Sophia.

Kijiji hicho pia kinakosa zahanati na hakuna kituo cha afya. Hivyo wanawake wengi hujifungulia nyumbani na kusababisha vifo vya watoto wakati wa uzazi na hakuna kumbukumbu za vifo zinazohifadhiwa.

Anasema “Sisi wanawake ndio tuna mzigo mkubwa. Mama unabeba mtoto mgong’oni, ndoo ya maji kichwani na furushi la nguo, kuja kutafuta maji.

“Maji yenyewe tunang’ang’aniana, ili kufika kwenye maji tunatembelea mikono, sehemu nyingine tunatembelea matako. Maji ni machafu. Ngedere, kwale, fisi, mbwa, ng’ombe na mbuzi wanaogelea, kunywa na kunya ndani ya haya maji,” analalama.

George Mwanahewa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilota, anasema yeye na wananchi hawajawahi kushiriki katika mipango ya bajeti na kuibua vipaumbele vya maendeleo ya kijiji chao.

“Nimekuwa kiongozi wa kijiji tangu mwaka 1992. Kwa muda wote huo ni mwezi Machi mwaka huu (2013) ndio tumepata fedha kutoka Kata kiasi cha Sh. 430,000. Kati ya fedha hizo Sh. 215,000 tuliambiwa zifanye maendeleo ya kijiji na tumekarabati choo cha wanafunzi. Zilizobaki ni matumizi ya ofisi.

Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Diwani wao, Fabian Mwakasole, na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mchungaji Luckson Mwanjale, katika kukabiliana na kero zinazokisibu kijiji, Mwanahewa alisema wote hawajarudi kijijini hapo baada ya uchaguzi wa 2010.

“Hakuna mkutano walioitisha katika muda wote huo. Nina maana hawajawahi kushukuru wananchi kuwa kuwapa ridhaa ya kuongoza. Wala hawashiriki tunapoitisha mikutano ya kijiji. Hapa kijijini hatujawahi kupata ugeni wa kiongozi yeyote. Tukishawapa kura huwa wanatoweka.”

Diwani Mwakasola amekiri kwamba Ilota yapo matatizo mengi, na la maji ni sugu. Ila wananchi wako bize sana, amejaribu mara mbili kuitisha mikutano hakufanikiwa.

Kata ya Mshewe ni moja ya kata ambako programu ya Maji na Usafi wa Mazingira itatekelezwa katika kijiji cha Mshewe, kimoja ya vijiji 17 vilivyomo eneo la programu hiyo.

Ripoti ya mwaka 2013 ya Halmashauri hiyo inasema kwa awamu ya kwanza ya programu, mwaka 2011-2012 katika vijiji vya Shongo, Igale na Iwalanje na bajeti yake ilikuwa Sh. 1.5 bilioni. Awamu ya pili 2012-2013 vijiji vya Idimi, Haporoto, Horongo, Swaya na Mbawi kwa bajeti ya Sh. 596 milioni.

Awamu ya tatu (2013-2014) itahusu vijiji vya Galijembe, Itimu, Iwindi, Izumbwe na Lupeta na bajeti yake ni Sh. 1.3 bilioni na awamu ya mwisho (2014-2015) itahusu vijiji vya Mwampalala, Mwashiwawala, Jojo na Mshewe.

Kulingana na mpango wa miaka mitano (2011-2015) wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kijiji cha Ilota hakimo katika mpango wa usambazaji wa maji safi na salama.

“Tunafanya juhudi kutafuta chanzo kingine cha fedha kitakachosaidia kuondoa tatizo la maji kijijini. Hali hii haiwezekani kuendelea hivihivi,” anasema Mashaka Sinkala, Kaimu Mhandisi wa Maji wa Halmashauri.

error: Content is protected !!