Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mahakama yawarejesha Mbowe, Matiko uraiani
Habari za SiasaTangulizi

Mahakama yawarejesha Mbowe, Matiko uraiani

Spread the love

MAHAKAMA Kuu kanda ya Dar es Salaam, imewarejesha uraiani wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (Hai) na Esther Matiko (Tarime Mjini). Anaripoti Faki Sosi …(endelea).

Mbowe na Matiko, walikuwa gerezani tokea tarehe 30 Novemba mwaka jana, kufuatia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ya Wilbard Mashauri, kuamua kuwafutia dhamana, kwa madai kuwa walikwenda kinyume na maelekezo ya mahakama.

Wakati Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa chama hicho akifuatiwa dhamana kwa madai ya kuidanganya mahakama kwa kusafiri kuelekea Marekani, huku akieleza kuwa alikwenda Afrika Kusini, Matiko alishindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa.

Wote wawili wanashitakiwa kwa makosa ya 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia; kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya 1 Februari na 16 Machi, mwaka jana, maeneo ya Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo, ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iriga Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Kibamba na Katibu wa Chadema, Tanzania Bara, John Mnyika.

Wapo pia, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya; Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, wanasiasa hao wawili, waliwasilisha rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Novemba mwaka jana.

Hata hivyo, maombi hayo ya rufaa hayakusikilizwa wakati huo, kutokana na serikali kuwasilisha rufaa ya Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa mahakama Kuu, kutupa maombi yao ya awali.

Kupitia mawakili wao, Peter Kibatara na Jerimiah Mtobyesya, Mbowe na Matiko, waliomba mahakama kuu kufuta wa uamuzi wa hakimu Mashauri kwa kuwa haukujielekeza kwa mujibu wa sheria.

Akisoma uamuzi uliowarejeshea dhamana washitakiwa hao, Jaji wa Mahakama Kuu, Sam Rumanyika amewaeleza mamia ya watu waliofurika mahakamani hapo kuwa maamuzi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hayakuwa sahihi.

Katika uamuzi wake huo, Jaji Rumanyika amesema, “kuwafutia dhamana washitakiwa kabla ya kutwaa mafungu ya dhamana ya wadhamini, ilikuwa ni sawa na kuweka Mkokoteni mbele ya Unga, badala ya kuweka Unga kwenye Mkokoteni.”

Alisema, “mamlaka za kuamua dhamana zipo kwa mujibu wa sheria, hata kama zinaweza kutumiwa kwa ustawi na kwamba masharti ya dhamana yanapaswa kuwa rahisi kwa watuhumiwa wote, ili kutoa ama kunyima dhamana kuwe na matokeo sawa.”

Aidha, Jaji Rumanyika amesema, ni kinyume cha sheria na “hatari zaidi, pale mahakama inapofuta dhamana bila kutoa sababu za msingi.”

Ameongeza, “dhamana ni faraja na anayeitoa hapaswi kuitwaa pale anapojiamua kwa matakwa yake binafsi. Kwa misingi hiyo, watuhumiwa Mbowe na Matiko, wana haki ya kupata dhamana.”

Jaji Sam Rumanyika Katika kufuta uamuzi wa mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana Freeman Mbowe na Esther Matiko ametaja misingi 9 ya Mahakimu kuzingatia Katika Maombi ya dhamana.
  • Kesi inadhaminika
  • Kutoa dhamana ni tafsiri dhahiri ya mahakama ya dhana ya katiba ya kuwa mtu hana hatia mpaka mahakama itakapomhukumu vinginevyo.
  • Kufuta dhamana kunahitaji sababu kubwa kuliko sababu za kumpa mtu dhamana
  • Mahakama izingatie Ukubwa wa kosa Kutoa masharti ya dhamana
  • Masharti ya dhamana yawekwe bila kuleta hisia kuwa mpango ni kunyima mtu dhamana.
  • Mahakama izingatie adhabu kwa makosa yaliyopo mbele yake ili Pale ambapo mshatikiwa akitiwa hatiani asiwe amedhibiwa mara 2.
  • Sababu ziwe zinakubalika mahakama yeyote duniani
  • Mahakama izingatie Msongamano uliopo gerezani na je kutoa dhamana au kufuta dhamana kunachangia au kupunguza msongamano gerezani
  • Mahakama izingatie kuwa Uhuru ya mshatakiwa hauna mbadala.
Jaji Rumanyika sio tu amewaachia huru Mbowe na Matiko bali pia amefuta masharti ya dhamana ya kuripoti Polisi kila wiki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!