November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yatupa pingamizi lingine la kina Mbowe

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania, imekubali kupokea hati ya ukamataji mali wa washtakiwa Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya iliyowasilishwa na shahidi wa nane, Jumanne Malagahe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru-Arusha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Uamuzi huo wa kupokea hati hiyo, umetolewa leo Jumanne, tarehe 9 Novemba 2021 na Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Halfan Hassan Bwire.

Ni baada ya jana Jumatatu, mawakili wa utetezi kuweka pingamizi kupinga hati hiyo ya ukamataji mali isipokelewe kwani imenukuu sheria ambayo haipo nchini huku mawakili wa jamhuri wakitetea kwamba mapingamizi hayo hayana mashiko.

Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo, Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo inatupilia mbali pingamizi hilo kwa kuwa upande wa utetezi haujaathirika kutokana na kifungu hicho kunukuliwa kimakosa pia, una nafasi ya kumuuliza maswali shahidi huyo mahakamani hapo.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo inaipokea hati hiyo kama kielelezo cha ushahidi namba 11 cha upande wa mashtaka.

“Kama inavyoonekama nyaraka ina makosa lakini yanaweza tibika. Mahakama imeona katika mazingira ya shauri hili, utetezi hawajaeleza kama wameathirika na kufungu kunukuliwa kimakosa na upande wa utetezi watapata nafasi ya kumuuliza shahidi hivyo inatibika na mahakama hii inapokea hati hiyo kama kielelzo namba 11,” amesema jaji Tiganga.

Uamuzi wa mahakama hiyo umetolewa baada ya jana, mawakili wa pande zote mbili kuvutana vikali kuhusu hati ya ukamataji mali za watuhumiwa hao.

Mabishano hayo yaliibuka kutokana na kifungu cha sheria kilichotumika katika hati hiyo, kukosewa kutamka.

Upande wa utetezi, ulidai kuwa kifungu cha 38 (3) cha Sura ya 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ilyofanyiwa marekebisho 2018, kilichotumika katika hati hiyo, hakipo katika sheria za nchi, kwa kuwa sheria hiyo hakikufanyiwa marekebisho mwaka huo.

Lakini upande wa jamhuri ulipinga hoja hiyo ukidai haina mashiko kwa mujibu wa sheria ya kutafsiri sheria, inayoelekeza namna ya kutamka sheria.

Ulidai kuwa, kwa mujibu wa sheria hiyo ya kutafsiri sheria, kifungu hicho cha sheria ni halali kwa kuwa sheria husika ilitamkwa licha ya mwaka kukosewa.

Hii ni mara ya tano kwa mahakama hiyo kutupa mbali mapingamizi yanayowekwa na mawakili wa Mbowe na wenzake, ambapo tarehe 20 Oktoba 2021, ilitupa pingamizi lao dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa, yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka, wakidai maelezo hayo yalichukuliwa kinyume cha sheria.

Pingamizi hilo lilitupwa na mahakama hiyo mbele ya Jaji Kiongozi Mustapha Siyani, kabla ya kujitoa kusikiliza kesi.

Pingamizi lingine dhidi ya mamlaka ya mahakama hiyo ya uhujumu uchumi kusililiza mashtaka ya ugaidi na hati ya mashtaka kuwa na makosa ya kisheria yalitupwa na Jaji Elinaza Luvanda, tarehe 1 Septemba mwaka huu, kabla ya kujitoa.

Pimizi jingine lilitupwa tarehe 1 Novemba 2021 na Jaji Tiganga kuhusu usahihi wa saini ya shahidi wa nne wa Jamhuri, Anita Mtaro (45), mfanyabiashara wa mbege, Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimamnajro.

Upande wa utetezi, walitaka shahidi huyo asaini pembeni ili kulinganisha saini alizokuwa amesaini katika fomu zilizotumika kujaza vitu walivyokutwanavyo Kasekwa na Lingw’enya mara baada ya kukamatwa Rau Madukani.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!