May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yatoa maagizo kwa wasikilizaji kesi ya Mbowe kuhusu shahidi

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imewaamuru watu waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, wamuache atoe ushahidi wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amri hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 28 Januari 2022, mahakamani hapo na Jaji Joachim Tiganga, wakati Wakili wa utetezi, John Mallya, anamuuliza maswali ya dodoso shahidi wa 12 wa Jamhuri, Luteni Denis Urio.

“Nyie ni wasikilizaji muacheni shahidi atoe ushaidi, naomba mumuache shahidi atoe ushahidi tunaelewana?” Alisema Jaji Tiganga ambapo wasikilizaji walijibu “sawa.”

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Jaji Tiganga alitoa amri hiyo kufuatia baadhi ya watu waliokuwa katika kesi hiyo, kuangua kicheko huku wengine wakinong’ona, baada ya Luteni Urio kusita kujibu swali la Wakili Mallya.

Wakili Mallya alimhoji, kwa nini hakutoa ufafanuzi juu ya sababu za jina la Free kutoonekana katika meseji zinazodaiwa kuwa ni mawasiliano yake na Mbowe, yaliyofanyika katika mtandao wa kijamii wa Telegram.

Luteni Urio alijibu swali hilo akidai kwamba, yeye anafahamu namba iliyotumika katika meseji hizo ni ya Freeman Aikaeli Mbowe.

Lakini Wakili Mallya hakuridhishwa na jibu hilo na kumuomba Jaji Tiganga amuamuru Luteni Urio, ajibu swali lake kama alivyomuuliza, ndipo Jaji huyo akamuelekeza shahidi huyo wa Jamhuri ajibu swali kama lilivyoulizwa.

Kufuatia maelekezo hayo, Luteni Urio alijibu akidai ufafanuzi huo hakuutoa, jibu lililowafanya baadhi ya watu waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo kuangua kicheko.

Luteni Urio anaendelea kutoa ushahidi wake, aliouanza juzi Jumatano, ambapo katika ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, alidai Mbowe alimtumia Shilingi 699,000 kumtafutia makomando wa JWTZ waliostaafu au kufukuzwa jeshini, kwa ajili ya kumsaidia katika harakati za chama chake kuchukua dola 2020.

Luteni Urio alidai kuwa, aliwasiliana na Mbowe kupitia mitandao ya kijamii ya Telegram, WhatsApp, meseji za kawaida pamoja na kupigiana simu huku akidai mwanasiasa huyo kuna wakati alikuwa anatumia namba ambazo si za kwake.

error: Content is protected !!