Saturday , 15 June 2024
Home Habari Mchanganyiko Mahakama yamtia hatiani Bosi wa Vodacom 
Habari Mchanganyiko

Mahakama yamtia hatiani Bosi wa Vodacom 

Hisham Hendi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania (katikati) akiwa mahakamani Kisutu
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini Sh. 5.8 bilioni, Hisham Hendi, Mkurugenzi  Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, baada ya kumkuta na hatia ya  kuisababishia Serikali hasara. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Hendi, raia wa Misri ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Tala na wafanyakazi wake wanne ambao ni raia wa Kenya wamehukumiwa adhabu hiyo kwa kusimika vifaa vya mawasilino bila kibali cha mamlaka husika.

Washtakiwa licha ya kuisababishia serikali hasara, pia walishtakiwa kwa kuhujumu uchumi na kuruhusu laini za simu 813 za Vodacom ambazo hazijasajiliwa  kutumika. 

Washtakiwa wamehukumiwa  baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yanawakabili kufuatia upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi dhidi ya washtakiwa hao umekamilika na washtakiwa kusomewa mashtaka upya.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi amesema, katika shtaka la kwanza hadi la sita washtakiwa, Ngassa, Lusiola na kampuni ya Inventure/ T/A Tala Tanzania wanahukumiwa kulipa faini ya Sh. 5 milioni kila mmoja katika kila shtaka na iwapo watashindwa basi watatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Katika shtaka la saba, washtakiwa, Ngassa, Luisola na Tala wamehukukiwa kulipa Sh. 642,276,000  ambazo waliisababishia TCRA hasara kwa kutumia laini 813 za Vodacom ambazo hazijasajiliwa na wakishindwa watarudishwa mahakamani kupangiwa adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.

Aidha katika shtaka la nane, washtakiwa Hendi, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Kampuni ya Vodacom wamehukumiwa kulipa faini ya Sh. 5 milioni kila mmoja au kwenda jela miezi 12.

Katika shtaka la tisa washtakiwa hao wamehukumiwa kurejesha sh. 5,250,237,000 kama hasara waliyoisababisha kwa TCRA wakishindwa watarudishwa mahakamani kupangiwa adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.

Pia washtakiwa hao wamehukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh. 120 milioni na iwapo wakishindwa basi watatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Mbali na Hendi, washtakiwa wengine waliohukumiwa ni Joseph Nderitu, Mkuu wa Kitengo cha Mapato Vodacom, Olaf Mumburi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Vodacom, Joseph Muhere, Mkuu wa Mauzo wa Vodacom na Meneja Mhasibu Ibrahim Bonzo.

Wengine ni Ahmed Issa ambaye ni Meneja Uendeshaji wa Biashara wa kampuni ya Inventure Mob Tanzania Ltd na Brian Lusiola ambaye ni mtaalamu wa IT.

Mapema kabla ya kusomewa adhabu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Jackline Nyantori aliiiomba mahakama kutoa adhabu kali ambayo itakuwa  fundisho kwao na kwa wengine wanaotenda makosa kama haya au wanaotarajia kutenda makosa kama haya.

Nao washtakiwa wakijitetea kupitia wakili wao Seni Malimi waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu washtakiwa kwani ni wakosaji wa kwanza.

Hata hivyo, washtakiwa wamelipa faini na kurejesha fedha hizo na kunusurika kwenda rumande.

Awali ilidaiwa, kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2018, huko katika jengo la Tanzanite Park, lililopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa Ngasa, Lusiola na kampuni ya Tala Tanzania  waliingiza kifaa cha mawasiliano kinachoitwa Proliant MLI GEN 9 Server (PABX Virtual Mashine yenye serial number 76520D88838129_425) bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Washtakiwa wanadaiwa pia kusimika kifaa hicho na kuendesha mtambo huo wa mawasiliano bila kuwa na leseni inayotolewa na TCRA.

Aidha  washtakiwa wanadaiwa, kutoka Januari 2 hadi Machi 11,2019 waliendesha kifaa hicho cha kieletroniki cha mawasiliano kwa kurusu simu za kimataifa zilizoingia nchini bila kibali cha TCRA.

Pia imedaiwa kati ya Aprili 17, 2018 na Machi 11, 2019 washtakiwa waliendesha mitambo hiyo kwa kupokea na kusambaza upokeaji wa simu za kimataifa bila kuwa na leseni hiyo.

Katika shtaka la tano inadaiwa kati ya Aprili 17, 2018 na Machi 11, 2019, mwaka huu, washtakiwa walikwepa kodi ya kupokea na kusambaza huduma ya upokeaji wa simu za kimataifa kwa kusambaza mawasiliano kwa kutumia mfumo huo.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa Aprili 17, 2018 na Machi 11, 2019, mwaka huu kinyume na sheria, washtakiwa walitumia vifaa vya mawasiliano kuunganisha  huduma ya kieletroniki ya mawasiliano kwa lengo la kupokea na kusambaza mfumo wa mawasiliano bila kupata kibali cha TCRA.

Imeendelea kudaiwa kuwa, katika tarehe hizo, maeneo ya Tanzanite Park Building Kinondoni, Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Tala, walitumia namba 813 za Vodacom ambazo ni namba maalum bila kupewa na TCRA.

Ngassa, Lusiola na Tala, pia wanadaiwa katika tarehe hizo, waliisababishia TCRA hasara ya Sh 642.2 milioni.

Katika shtaka la Tisa, Wakili Wankyo Simon amedai kuwa Hendi, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Kampuni ya Vodacom, kati ya Aprili 17, 2018 na Machi 11, 2019, mwaka huu maeneo ya jengo la Vodacom, lililopo Ursino Estate barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam, waliwaruhusu  Ngassa, Lusiola na Tala kutumia namba 813 za Vodacom bila kuzipata kutoka TCRA.

Pia Simon alidai washitakiwa hao kutoka Vodaom katika tarehe hizo, kwa pamoja waliisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh. 5,250,237,000.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

DAWASA yaja na suluhisho la maji kwa wakazi wa Sinza C,D

Spread the loveWakazi wa Kata ya Sinza, Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Vitalu 19 vya madini vyazalisha ajira 12,000 Songwe

Spread the loveZAIDI ya vijana 12,000 kutoka Wilaya ya Songwe mkoani Songwe...

Habari Mchanganyiko

Mmoja auawa kwa tuhuma za kuiba sokoni, Polisi walaani

Spread the loveMwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina lake  ameuawa  na wananchi wenye...

error: Content is protected !!