August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yamtema Kafulila

David Kafulila, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi

Spread the love

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora leo mbele ya Jaji David Mrango, imefuta ombi la David Kafulila la kuingiza rufaa yake upya, anaandika Pendo Omary.

Kafulila alitaka kuingiza rufaa yake upya ili apate fursa ya kuiingiza katika Mahakama ya Rufaa fomu za tume No 21B za kila kituo kwenye vituo vyote 382 kusomwa matokeo yake kubaini mshindi tofauti na ilivyokuwa katika ngazi ya Mahakama Kuu.

Hatua ya kufutwa rufaa hiyo inakuja baada ya Mahakama ya Rufaa tarehe 13 Oktoba mwaka huu mbele ya majaji Luanda Bernad, Mbarouk Salim na Mziray Richard kushindwa kuondoa rufaa hiyo na kuelekeza kuwa, rufaa hiyo inaweza kurejeshwa baada ya marekebisho.

Katika ombi hilo, Kafulila alitaka mahakama kuu kwa mujibu wa sheria imruhusu aingize rufaa hiyo upya kwa kuwa ni haki ya kisheria.

Hata hivyo Jaji Mrango katika uamuzi wake amesema kwamba, maombi ya Kafulila yamekosa hoja za msingi kuishawishi mahakama kuu kuruhusu rufaa hiyo kuingizaa upya kama alivyoomba.

Kwa upande wake Kafulila ameeleza kutoridhika na uamuzi huo kwa hoja kwamba, sababu za kuingiza rufaa hiyo upya zipo wazi kuwa, rufaa ya awali ilitupwa kabla ya kusikilizwa, hivyo sababu za kutaka rufaa hiyo ingizwe upya ni ili rufaa iweze kupata kusikilizwa na kuamuliwa.

“Nasikitishwa na vigingi hivi kwa hoja kwamba kesi hii inahusu nani aliyepata kura nyingi na tume imeleta fomu mahakamani na zinaonesha aliyetangazwa sio aliyeshinda lakini bado mahakama haioni sababu ya kutoa haki hiyo,” amesema Kafulila.

Kafulila amesema anatafakari na wakili wake kisha atamua ndani ya siku chache.

error: Content is protected !!