August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yaizima NHC sakata la Mbowe

Spread the love

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi imeliamuru Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutouza au kupiga mnada mali za Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mpaka kesi ya msingi itakapomalizika, anaandika Faki Sosi.

Shirika hilo lilizichukua mali mbalimbali za kampuni za Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, wiki iliyopita kupitia mawakala wa kampuni ya Fosters Auctioneers katika jengo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya NHC ilitokana na mgogoro wa muda mrefu, wakimtuhumu Mbowe kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 1.3 bilioni, ikiwa jumla ya fedha za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo.

Kutokana na mvutano huo, Mbowe alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kupinga hatua ya NHC kumuondoa katika jengo hilo, pamoja na kuchukua mali zake huku wakitangaza kuzipiga mnada baada ya siku 14 tangu kuzichukua.

Leo, Jaji Siyovelwa Mwangasi ametoa zuio na kuiamuru NHC kutouza wala kupiga mnada mali hizo za Mbowe mpaka mahakama hiyo itakapotolea uamuzi katika kesi ya msingi.

Katika kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili na Peter Kibatala na Omary Msemo.

Jaji Mwangasi amesema kuwa, anakubaliana na maombi ya mlalamikaji na kutaka mali hizo zisiuzwe hadi hapo mahakama itakapofanyia uamuzi kesi ya msingi.

Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa NHC kupitia mawakili wake Aloyce Sekule na Miriam Mungula kushindwa kuwasilisha hoja za msingi kueleza, ni kwanini zuio hilo lisitolewe hadi hapo kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa.

Awali, mawakili wa NHC, walidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya Mbowe kwa kuwa hakuna kesi ya msingi ambayo imefunguliwa, hivyo maombi hayo yatupiliwe mbali.

Huku wakili Kibatala akijibu hoja hiyo kwa kusema, hatua ya kuwasilisha maombi hayo inalenga kubaini kama kweli Mbowe anadaiwa kodi ama la.

Kibatala amedai kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza ikatoa uamuzi wowote, na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili itolewe amri ya muda ya kuzuia mchakato huo.

Miongoni mwa hoja za Mbowe alizoziwalisha mahakamani hapo, ni pamoja na hoja kuwa, yeye (Mbowe) na shirika hilo walikubaliana kwamba atakarabati na kulipanua jengo hilo kwa gharama zake kwa asilimia 100. Makubaliano ambayo yaliingiwa mwaka 1997.

Amedai kuwa katika makubaliano hayo yeye na NHC walikubaliana watamiliki jengo hilo kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku Mbowe katika mgawanyo wa mapato akitakiwa kupata asilimia 75 na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.

Pia ameleza kuwa katika makubaliano hayo, licha ya mwenendo wa kibiashara kutokuwa mzuri, muda wote alikuwa anajitahidi kulipa kwa mujibu wa makubaliano yao.

Hivyo kutokana na hatua ya NHC kuvunja mkataba huo kwa kumtoa kwenye jengo na kuchukua mali zake, anaiomba mahakama iliamuru shirika hilo limlipe fidia.

Mbowe aliondolewa kwenye jengo husika mnamo Septemba mosi kwa madai ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 1.3.

Mawakala wa NHC walifika katika jengo hilo saa 12:30 asubuhi na wafanyakazi zaidi ya 50 na kwenda moja kwa moja katika kampuni ya Free media pamoja na ukumbi wa Bilcanas na kuchukua vifaa mbalimbali ikiwemo, meza, viti na kompyuta.

Siku chache baada ya kuondolewa kwa Mbowe katika jengo hilo, Rais John Magufuli alilisifu shirika hilo kwa hatua hiyo na kulitaka lichukue hatua kama hizo kwa wadaiwa wengine zikiwemo taasisi za umma.

 

error: Content is protected !!