July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yafuta hukumu ya Mbowe, kurejeshewa mamilioni

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

HUKUMU ya kesi ya Jinai Na. 112/2018 iliyotolewa na Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliyomuhusu Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake saba, imebatilishwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ndiyo iliyobatilisha hukumu hiyo na kuamuru Mbowe na wenzake warejeshewe fedha zao kiasi cha Sh.350 milioni walizolipa kama faini.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, tarehe 25 Juni 2021 na jaji wa mahakama hiyo, Irvin Mgeta, akisoma hukumu ya Rufaa Na. 76/2020, iliyowasilishwa na Mbowe na wenzake, kupinga hukumu hiyo iliyotolewa tarehe 10 Machi 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mbali na Mbowe, warufani wengine katika rufaa hiyo ni, Katibu Chadema, John Mnyika na Naibu Katibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu.

Wengine ni waliokuwa wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Akizungumza baada ya uamuzi huo, wakili upande wa warufani, Peter Kibatala, amesema, Jaji Mgeta ameamuru warufani hao warejeshewe fedha zao.

Pia wakili huyo amesema, amri hiyo inamfaidisha Vicent Mashinji, ambaye hakukata rufaa.

“Ameamuru faini zote ambazo warufani walilipa irejeshwe kwao, amri hizo zinamfaidisha pia mshtakiwa Vicent Mashinji,  ambaye hakukata rufaa, lakini jaji amesema pamoja na kwamba hakukata rufaa.

“lakini anatumia mamlaka yake kisheria ana amrisha sio tu kwamba hana hatia katika mashtaka yote aliyotiwa hatiani, lakini anafaidika na amri ya kurejeshewa faini alizolipa,” amesema Kibatala.

Kibatala amesema, baada ya hukumu hiyo, wanaanza mchakato wa kudai fedha hizo za faini.

“Tunaanza mchakato wa kudai faini, lakini wateja wangu rekodi zao za kushtakiwa zimefutwa leo.  Ilikuwa safari ndefu lakini mambo ya kisheri unatiwa hatiani hapa,  hukati tamaa unakata rufaa hatimaye unafanyika usafishaji kama huu,” amesema Kibatala.

error: Content is protected !!