December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yaelezwa sababu mwenzake Mbowe kuhamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni

Spread the love

 

MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilayani Arumeru, Arusha, SP Jumanne Malangahe, ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kuwa walimhamishia Mohammed Abdillah Ling’wenya, Kituo cha Polisi Mbweni Dar es Salaam kutoka kituo kikuu cha polisi mkoani humo. Anaripori Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

SP Jumanne amesema hayo leo Alhamisi tarehe 11 Novemba 2021, mahakamani hapo, akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya Ling’wenya, yasipokelewe katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake.

Shahidi huyo wa jamhuri alitaja sababu hiyo, baada ya upande wa utetezi kudai kwamba, Ling’wenya alipokuwa katika Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani Dar es Salaam, alilazimishwa kusaini karatasi iliyodaiwa kuwa na maelezo yake, bila kuyasoma.

Na kwamba SP Jumanne alimtishia kuwa, asipoisaini atampa mateso kama aliyopewa alipokuwa Kituo cha Polisi cha Kati Moshi, Kilimanjaro.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake, SP Jumanne alidai alimfanyia mahojiano Ling’wenya pamoja na kuandika maelezo hayo ya onyo, tarehe 7 Agosti 2020, katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam na kwamba mtuhumiwa huyo alisaini kwa hiari yake karatasi hiyo akiwa kituoni hapo.

Mahojiano ya Wakili Kidando na SP Jumanne yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili Kidando: Baada ya zoezi la kuandika maelezo ya Ling’wenya, elezea ni wakati gani ulikutana naye tena baada ya tarehe 7 Agosti 2020.

Shahidi: Baada ya kumaliza shughuli yangu tarehe 7 Agosti 2020 niliondoka kituoni hapo kuendelea na majukumu mengine, niliyoelekezwa na ACP Ramadhan Kingai (aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoani Arusha), mpaka tarehe 8 Agosti 2020, ACP Kingai alinielekeza nikiwa na Inspekta Mahita kuwahamisha watuhumiwa hao kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbweni.

Asubuhi majira ya saa tano asubuhi, nilimuelekeza Inspekta Mahita awachukue watuhumiwa hao katika Chumba cha Mashtaka, watuhumiwa walikuwa wawili, (Ling’wenya na Adam Kasekwa),

Wakili Kidando: Baada ya kumuelekeza Inspekta Mahita watuhumiwa walikuwa wapi?

Shahidi: Watuhumiwa walikuwepo palepale, niliwaingiza kwenye gari tukiwa tunashuhudia kisha kuanza safari ya kuelekea Kituo cha Polisi Mbweni.

Wakili Kidando: Ukiacha watuhumiwa wawili nani aliungana na nyie kwenye gari?

Shahidi: Ukiacha hao watuhumiwa wawilo tulikuwa na Inspekta Mahita, Swilla, Detective Constable Goodluck pamoja na dereva wa gari.

Wakili Kidando: Mlitumia muda gani kutoka Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam hadi Kituo cha Polisi Mbweni?

Shahidi: Tulitumia dakika 45, tulikuwa na gari yenye kimurimuri ilikuwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakili Kidando: Njiani kitu gani kiliendelea kati yenu na mtuhumiwa Ling’wenya?

Shahidi: Tukiwa njiani hakuna chochote kilichoendelea kati yetu.

Wakili Kidando: Nini kiliendelea Mbweni?

Shahidi: Baada ya kufika Mbweni watuhumiwa niliwapeleka kaunta ambapo pia nilisimama pembeni nikamuelekeza Inspekta Mahota awakabidhi katika chumba cha Mashtaka.

Baada ya kuwakabidhi sisi tuliondoka kuendelea na shughuli za upelelzi kufuatilia watuhumiwa wengine.

Wakili Kidando: Elezea wakati gani ulikutana na Ling’wenya baada ya tarehe 8 Agosti 2020?

Shahidi: Baada ya siku ya tarehe 8 Agosti 2020, sikuwahi kutana tena na mtuhumiwa huyo.

Wakili Kidando: Elezea kwa ufahamu wako vituo vya polisi alivyoletwa Ling’wenya baada ya kufika Dar es Salaam?

Shahidi: Kwa ufahamu wangu vituo alivyofikishwa Ling’wenya baada ya kufika Dar es Salaam, ni viwili, Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam na Kituo cha Polisi cha Mbweni.

Wakili Kidando: Hakuna kilichofanyika zaidi ya kumkabidhi Ling’wenya, elezea sababu za kumtoa Kituo cha Polisi Kati Dar ea Salaam kumpeleka Kituo cha Polisi Mbweni?

Shahidi: Sababu hasa za kumtoa Ling’wenya kutoka Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam, kwenda Kituo cha Polisi cha Mbweni, ilikuwa za kiupelelezi, ilikuwa kuepuka muingiliano wa watuhumiwa wengi.

Kuingia na kutoka kituoni hapo, ni kitu ambacho tuliona taarifa zingefika kwa watuhumiwa wengine tuliokuwa tunawatafuta hivyo wangekimbia kabisa.

Wakili Kidando alimuuliza shahidi huyo kuhusu tuhuma za kumtishia Ling’wenya ili asaini nyaraka ya maelezo hayo, kama ifuatavyo;

Wakili Kidando: Katika mapingamizi yake alichokisema ulimtishia kwamba yale mateso aliyopatiwa Moshi yataendelea kama hata saini maelezo ambayo hakuyasema?

Shahidi: Sio kweli, sikuwahi mtishia mahali popote pale mwani alikuwa na ushirikiano na sikuwa na sababu yoyote ya kumtishia.

Sikumtishia katika Kituo cha Polisi Mbweni kama alivyodai, kwani maelezo aliandika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam.

Baada ya kujibu swali hilo, SP Jumanne aliyatambua maelezo hayo na kuiomba mahakama iyapokee kwa ajili ya utambuzi.

Jaji Tiganga alikubali kuyapokea kwa ajili ya utambuzi.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa taarifa na habari mbalimbali

error: Content is protected !!