November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yaelezwa Mbowe alivyogoma kuandika maelezo polisi

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam, imeelezwa namna Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alivyogoma kuandika maelezo ya onyo dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es salaam…(endelea).

Mahakama hiyo imeelezwa hayo leo Jumanne, tarehe 9 Novemba 2021 na Mkuu wa Upelelezi wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha, SP Jumanne Malangahe, akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joackim Tiganga.

SP Jumanne ametoa madai hayo, akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, ambapo alidai Mbowe alikataa kutoa maelezo hayo kesho yake tarehe 22 Julai 2021, katika Ofisi ya mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZCO), mbele ya Mwanasheria wake, Fredrick Kihwelo.

Mbowe na wenzake watatu ambao ni Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya wanakabiliwa na tuhuma za kupanga vitendo vya kigaidi kwa kulipua vituo vya mafuta katika maeneo kadhaa nchini.

Mahojiano yao yalikuwa hivi;

Wakili Kidando: Mbowe aliletwa wapi?

Shahidi: Tarehe 22 Julai 2021, ilipofika saa 6.51 usiku nilipokuwa kituoni hapo ndipo Mbowe aliletwa mbele yangu na Inspekta Machota.

Wakili Kidando: Inspekta Machota alikuwa eneo gani?

Shahidi: Alikuwa eneo la Kituo cha Polisi cha Kati, katika ofisi ya ZCO.

Wakili wa Serikali: Nini kiliendelea?

Shahidi: Baada ya kuwa ameletwa pale alinikabidhi mtuhumiwa huyo na hivyo alinitambulisna kwake kwa majina yangu na cheo changu.

Baada ya kujitambulisha nilimueleza kwamba, nataka kufanya naye mahojiano. Nilimuonya kwamba anatuhumiwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kugaidi, kinyume cha kifungu cha 24 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi.

Wakili Kidando: Ulimfahamisha nini kingine?

Shahidi: Na kwamba halazimishwi kusema lolote dhidi ya tuhuma hizi, isipokuwa kwa hiari yake mwenyewe na lolote atakalosema litaandikwa chini na linaweza kuwa ushahidi mahakamani.

Vilevile, nilimuelekeza kwamba anayo haki ya kuwepo mwansheria, ndugu, jamaa au rafiki yake, ili aweze kushuhudia wakati maelezo hayo yanaandikwa.

Wakili kidando: Baada ya kumfahamisna ulifanya nini?

Shahidi: Nilisani sehemu yangu na yeye akasaini sehemu yake na akajibu onyo hilo kuwa, ameonyqa kwamba anatuhumiwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

Pia, anajua haki yake ya kuwepo mwanasheria wake ili ashuhudie. Baada ya kujibu onyo nilisaini na yeye alisaini.

Hivyo nilimuelekeza kama yuko tayari kutoa maelezo yake akajibu ndiyo, nilimuuliza angependa nani awepo wakati maelezo yake yanaandikwa, akajibu kwamba angependa awepo mwanasheria wake ambaye alimtaja Ferdrick Kihwelo.

Wakili Kidando: Baada ya kueleza hayo ulifanya nini?

Shahidi: Nikamuita Inspekta aliyemleta afanye mawasiliano kumpata mwanasheria wake ili ashuhudie lakini ufuatiliani ulifanyika mwanasheria wake hakuweza kupatikana siku hiyo.

Wakili Kidando: Vipi kuhusiana na ufuatiliaji wa mwnasheria wake?

Shahidi: Kesho yake ndipo mwanasheria wake Fredrick Kihwelo alipofika kwenye ktuo cha polisi katika ofisi ya ZCO Kanda ya Dar es Salaam.

Wakili Kidando: Alivyofika wewe ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa kituo cha polisi yeye mtuhumiwa alikuwa ameshafika mara kidogo Fredrick alifika.

Wakili kidando: Mbowe alitokea wapi?

Shahidi: Sikujua sababu aliletwa mbele yangu na Inspekta Machota ambaye nilimkuta pale.

Wakili Kidando: Baada ya kufika nini kiliendelea?

Shahidi: Baada ya mwanasheria wake kufika niliendelea kujitambulisha mbele ya mtuhumiwa na mwanasheria wake nikaendelea kusoma tuhuma zinazomkabili.

Baada ya kurejea hayo, nilimuekeza mtuhumiwa tuendelee kuandika maelezo kama alivyoomba. Lakini alijibu kwamba hayuko tayari kutoa maelezo yake mbele ya afisa wa polisi.

Baada ya mahojiano hayo nilisaini na yeye alisaini.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Kidando alimuuliza anaiomba nini mahakama, akajibu akidai anaiomba mahakama hiyo ipokee nyaraka ya maelezo hayo ambayo ilipokelewa kama kielelezo.

Endelea kufuatilia MwaanHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kujua kinachoendelea ambapo ataanza kuhojiwa na upande wa utetezi

error: Content is protected !!