April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yachoshwa na danadana kesi ya Tito

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Februari 2020, imeagiza upande wa Jamhuri kueleza bayana hatua iliyofikiwa katika upelelezi wa kesi inayomkabili Tito Magoti na mwenzake. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo imetokana na upande wa Jamhuri kueleza mahakamani hapo mara kwa mara kwamba, upelelezi bado haujakamilika ama umefikia hatua nzuri.

Mahakama imetoa amri hiyo leo kufuatia ombi kutoka kwa jopo la mawakili wa utetezi, walioiomba mahakama hiyo kurejea maelezo yaliyotolewa na upande wa Jamhuri tarehe 7 Januari 2020, ambapo mawakili wa mashtaka waliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua nzuri.

Ombi la mawakili wa utetezi limekuja kufuatia hoja ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon kuiambia mahakama hiyo, kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa tu kwani upelelezi wake bado haujakamilika.

Kutokana na mvutano huo wa kihoja, hakimu wa mahakama hiyo Janeth Mtega amesema, mahakama yake ilitoa amri tarehe 5 Februari 2020, upande wa Jamhuri kuja kuieleza hatua iliyofikiwa katika upelelezi wa shauri hilo.

Hivyo, Jamhuri inapaswa kuheshimu amri ya mahakama na sio kudai, kwa ujumla kila mara kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa mpaka tarehe 4 Machi 2020.

error: Content is protected !!