Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mahakama Rufaa yabatilisha hukumu ya Mwalimu kunyongwa
Habari Mchanganyiko

Mahakama Rufaa yabatilisha hukumu ya Mwalimu kunyongwa

Kitanzi
Spread the love

MAHAKAMA ya Rufani nchini, imezuia utekelezaji wa hukumu ya kunyongwa hadi kufa, iliyokuwa imetolewa kwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Kibeta, iliyopo wilayani Bukoba, mkoani Kagera, Respicius Patric. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Mwalimu Respicius aliamriwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Kagera, kunyongwa hadi kufa, tarehe 6 Machi 2019, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ya Sperius Eradius (13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano, katika shule ya Kibeta.

Sperius alifariki dunia baada ya kukumbana na kipigo kutoka kwa mwalimu wake Respicius, baada ya kumtuhumu ameiba pochi ya mmoja wa walimu wa shule hiyo, aliyefahamika kwa jina la Herieth Gerald.

Katika uamuzi wake wa jana Jumatatu, Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu wamebaini dosari kadhaa zilizopo kwenye hukumu ya Mahakama Kuu na hivyo, kuelekeza kusitishwa kwa adhabu hiyo.

Majaji wa Mahakama ya Rufaani, Stella Mugasha, Lugano Mwandambo na Ignas Kitusi, wameeleza sababu za kusimamisha utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama Kuu, ni kushindwa kueleza ushahidi wa shahidi wa tatu na wa tano wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo ya Jinai, Na. 56 ya mwaka 2018, Mwalimu Respicius alishitwakiwa pamoja na mwalimu mwenzake, Herieth Gerald. Wote wawili walidaiwa kutekeleza mauaji hayo tarehe 27 Agosti 2018, kwa kutumia  fimbo na magongo.

Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashitaka na mashahidi waliokuwapo kwenye tukio hilo, pochi iliyodaiwa kuibiwa na Sperius ilirejeshwa kwa Mwalimu Herieth na dereva wa bodaboda, akieleza kuwa mhusika aliisahau kwenye chombo hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha, alimtia hatiani Mwalimu Respicius kwa kosa hilo na kuagiza kuwa anyongwe hadi kufa, huku Mwalimu Heriath akiachiwa huru kwa maelezo ya kukosekana ushahidi.

Mahakama ya Rufani kupitia jopo la majaji watatu ambao ni   Lugano Mwandambo, Ignas Kitusi na Stella Mugasha, waliamua kuanza kusikilizwa upya shauri hulo kutokana na dosari za kisheria zilizobainishwa.

Moja ya dosari zilizobainika kwenye shauri hilo ni pamoja na kushindwa au kuruka kuelezea ushahidi wa shahidi wa shahidi wa tatu na tano wa upande wa mashtaka.

Kasoro nyingine, ni Jaji Mlacha kutowalezea Wazee wa Baraza, jambo ambalo ni muhimu sana kwenye  viambatanisho muhimu vya kosa la mauaji ya kukusudia.

Aidha, majaji hao wameeleza kuwa ingawa Mahakama Kuu ilirejea dhana ya nia ya pamoja ya washtakiwa kutenda kosa, katika muhtasari wake, hakuwaelezea washauri wa mahakama maana ya nia ya pamoja kuhusianisha na kesi inayowahusisha watu wawili.

Katika uamuzi huo, Mahakama ya Rufani imesema, matokeo ya kasoro hizo ni kwamba, Wazee wa Baraza hawakuelezwa barabara ili waweze kutoa maoni yao kwa usahihi.

“Kwa maneno mengine ni kwamba, Wazee wa Baraza, waliondolewa haki yao ya kueleza maoni yao kama wanavyotakiwa chini ya kifungu cha 298(1) cha CPA,” imeeleza sehemu ya maamuzi ya majaji hao wa Mahakama ya Rufaa.

Vilevile, Majaji wa Mahakama ya Rufaa wamesema, kama walivyeoeleza kwa usahihi mawakili wa pande zote, haiwezekani kusema kuwa Mahakama Kuu iliendesha kesi hiyo kwa msaada wa Wazee wa Baraza kama inavyotakiwa na Kifungu cha 265.

Hivyo, Mahakama ya Rufani imesema, athari za tatizo hilo huufanya mwenendo wa kesi na matokeo yake, yaani hatia na adhabu, vyote kuwa batili.

wanafunzi wa Sperius, alifariki dunia tarehe 27 Agosti 2018, akidaiwa kipigwa na mwalimu wake kwa tuhuma za kuiba pochi ya Mwalimu Herieth.

Baadhi ya wanafunzi walioshuhudia tukio hilo walisema, mwanafunzi huyo alikwenda kumpokea mizigo mwalimu wake aliyefika shuleni hapo kwa usafiri wa bodaboda, lakini baada ya mwalimu huyo kuingia ofisini alianza kulalamika kutoiona pochi hiyo.

Wanafunzi hao walidai kuwa mwanafunzi mwenzao aliitwa na kuanza kuhojiwa kuhusu kupotea kwa pochi hiyo na akakana kuichukua, hali iliyosababisha kuanza kupigwa akitakiwa kuirejesha.

Wamesema kuwa baadaye walitakiwa kuitafuta pochi hiyo mpaka chooni, lakini hawakuiona huku mwanafunzi huyo akiendelea kuadhibiwa.

Taarifa zilieleza, wakati mwanafunzi mwenzao akiendelea kupigwa, dereva bodaboda alifika shuleni hapo akimtafuta mwalimu aliyepoteza pochi na kumkabidhi pochi aliyokuwa ameisahau kwenye pikipiki yake.

Mashuhuda hao walisema kuwa baada ya pochi hiyo kupatikana, mmoja wa walimu aliagiza mwanafunzi huyo apatiwe juisi na bagia, chakula ambacho hakuweza kukila kutokana na maumivu.

Ripoti ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera, Dk. John Mwombeki, ilikiri kupokea mwili wa mtoto huyo majira ya saa mbili asubuhi ukionekana kuwa na majeraha ya siku za nyuma.

Dk. Mwombeki amesema uchunguzi wa awali wa mwili wa mtoto huyo ulionyesha amefariki dunia kutokana na kipigo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!