Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mahakama yaliamuru gazeti la The Citizen kumlipa Mchechu Sh. 2.5 bilioni
Habari Mchanganyiko

Mahakama yaliamuru gazeti la The Citizen kumlipa Mchechu Sh. 2.5 bilioni

Nehemiah Mchechu, Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
Spread the love

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imeliamrisha gazeti la kila siku linalochapishwa kwa lugha ya Kiingereza nchini la The Citizen, kumlipa fidia ya Sh. 2.5 bilioni, Nehemia Nchechu, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Nyumba la taifa (NHC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo, umetolewa leo Ijumaa, tarehe 3 Machi 2023 na Jaji Leila Mgonya, ambapo amesema mleta maombi anastahili kulipwa kiasi hicho cha fedha, kwa sababu ya kuchafuliwa jina lake.

Amesema, katika adhabu hiyo, kiasi cha Sh. 2 bilioni, zimetolewa kwa ajili ya fidia ya kuchafulia jina na kumshushia heshima mbele ya jamii na Sh. 500 milioni, ni kwa ajili ya kumsababishia hasara ya jumla.

Mbali ya kiasi hicho cha fedha, The Citizen limeamuriwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi; kuandika habari ya kumwomba radhi katika ukurasa wake wa mbele kwa ukubwa ule ule na kulipa riba ya asilimia 12 kila mwaka, endapo litashindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kuanzia leo.

Aidha, Mahakama imelionya gazeti hilo kutomwandika tena mleta maombi kwa habari ya uongo na yenye kumchafulia jina kiasi hicho, isipokuwa ikiwa itajiridhisha na ukweli wa inachokiandika.

Mapema mwaka 2018, Mchechu alifungua shauri mahakamani hapo, akilituhumu gazeti la The Citizen kuchafua jina lake. Akataka mahakama iamuru gazeti hilo, limlipe fidia ya Sh. 3 bilioni na kuombwa radhi.

Mchechu ambaye aliondolewa kwenye wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa NHC na Rais Dk. John Magufuli, alirejeshwa kwenye nafasi hiyo mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, wiki iliyopita, aliondolewa tena kwenye nafasi hiyo kwa kufanywa kuwa Msajili wa Hazina.

Tarehe 23 Machi 2018, The Citizen liliandika katika ukurasa wake wa mbele, habari iliyobeba kichwa cha maneno: “Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu – kwa nini JPM alivunja bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu?

Habari hiyo ilitaja sababu kadhaa, kutoka vyanzo mbalimbali, ilieleza kuwa uamuzi wa Rais Magufuli, umetokana na Mchechu kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.

Gazeti lilisema, baadhi ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mchechu, zilikuwa zikichunguzwa na bodi ya NHC na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Miongoni mwa tuhuma hizo, ni kuwapo kwa mgongano wa maslahi katika ununuzi wa ekari 500 za mradi wa nyumba za shirika maarufu kama Safari City, jijini Arusha.

Vilevile, gazeti lilidai kuwa Mchechu anachunguzwa na Takukuru kwa madai ya kumtumia mkandarasi aliyekodishwa na NHC, kujenga barabara yake binafsi karibu na mradi huo wa Arusha.

Kuhusu mradi wa Kawe, gazeti hilo lilidai kuwa aliingia makubaliano na kampuni ya ukandarasi ya PHILS International yenye makao yake Falme za Kiarabu (Dubai), bila kushirikisha kitengo cha ununuzi wa NHC.

Hoja zingine zilizotajwa kwenye habari hiyo, ni kuhusu madai kuwa Mchechu anachunguzwa kwa tuhuma kuwa kampuni ya mwenza wake, kupewa zabuni ya kutoa huduma za bima kwenye nyumba za NHC mkoani Mtwara, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya viongozi wa umma.

Madai mengine, ni matumizi mabaya ya ofisi yaliyotajwa kuwa yametendeka kwa kiwango kikubwa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Leila alisema, upande wa washitakiwa umeshindwa kuleta ushahidi kuthibitisha ilichokiandika.

Alisema, Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na Mchechu, kwamba habari iliyoandikwa dhidi yake ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kumchafua.

Alisema, mashahidi wa upande wa utetezi Bernad James – mhariri wa habari za Mahakama na Thomas Masyoba, mhariri mtendaji – wameshindwa kuleta ushahidi kudhibitisha uhalali na usahihi wa habari waliyoichapisha.

“Mahakama inaheshimu vyanzo vya habari kama mashahidi walivyoeleza, lakini hakuna ushahidi wowote unaothibitisha, kile ambacho kimechapishwa.

“Kwa mfano, mashahidi wanasema, Mchechu alihojiwa na Takukuru au tume iliyoundwa kumchunguza, lakini yeye anasema hajawahi kuhojiwa na chombo chochote,” alisema Jaji Leila.

Alisema, mashahidi wa upande wa utetezi walisema, habari yao ni mwendelezo wa kauli aliyoitoa Rais Magufuli wakati akifungua nyumba za shirika hilo mjini Dodoma.

Alirejea ushahidi wa video ya taarifa ya Rais Magufuli iliyorushwa na kituo cha televisheni cha Azam na kuonyeshwa mahakamani, kwamba inaonyesha kuwa Rais Magufuli alisema kuna matumizi mabaya ya fedha ndani ya shirika, lakini hakutaja jina la mtuhumiwa.

Aliongeza, “lakini habari iliyoandikwa na gazeti la The Citizen, imeenda mbali na kuongeza mambo mengine ambayo Rais Magufuli hakuyasema na hayana Ushahidi.”

Jaji Leila alivitaka vyombo vya habari pamoja na taaluma zingine wakiwamo majaji, kutimiza majukumu yao na kulinda haki na hadhi za wananchi bila kuwavunjia heshima katika jamii.

Alisema, Mcheche ni mtu maarufu, mtumishi wa ngazi ya juu serikalini, yumo katika bodi mbalimbali na kiongozi wa kanisa, hivyo kwenye ushahidi wake alisema habari hiyo ilimshushia hadhi na kulazimika kujiuzulu nafasi zake katika maeneo mengi aliyokuwa akiyatumikia.

Katika shauri hilo, Mchechu alitetewa na mawakili Vitalis Peter na Aliko Mwamanenge, wakati The Citizen lilitetewa na Ambrose Nkwera na Raban Rugina.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!