Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mahakama Kuu: Magufuli alivunja katiba kumuondoa ofisini Prof Assad kama CAG
Habari za SiasaTangulizi

Mahakama Kuu: Magufuli alivunja katiba kumuondoa ofisini Prof Assad kama CAG

Spread the love

MAHAKAMA Kuu Tanzania leo tarehe 5 Disemba, 2022 imetoa uamuzi kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli alivunja Katiba alipomwondoa Prof. Mussa Assad kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Shauri hilo namba 8 la mwaka 2020, liliwasilishwa mahakamani hapo na Kiongozi mkuu wa ACT Waalendo, Zitto Kabwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzie. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Rais John Magufuli akimuapisha Charles Kichere kuwa CAG mpya tarehe 3 Novemba, 2019

Shauri hilo lililoamuliwa mbele ya jopo la majaji watatu Dk. Benhaj Masoud, Juliana Masabo na Edwin Kakolaki lilikuwa linapinga sheria iliyotumika kutenguliwa kwa Prof. Mussa Assad kama CAG na kuteuliwa kwa Charles Kicheere.

Aidha, kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Zitto, Mahakama Kuu imekubaliana na shauri hilo kuwa sheria iliyotumika ni batili.

Kwamba ukomo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali umewekwa na Katiba na Sheria iliyoweka muhula inapingana na Katiba. Prof. Mussa Assad alipaswa kuhudumu kama CAG mpaka umri wa kustaafu ufike Kwa Mujibu wa Katiba.

“Nimefarijika sana kuwa Mahakama Kuu imesimama na Katiba katika shauri hili. Kwamba sasa haitatokea tena kwa Mtu mmoja Hata kama ni Rais kuamua tu kuvunja Katiba ya Nchi yetu atakavyo. Muhimu zaidi ni kwamba kwa hukumu hii ma CAG wote wajao katika nchi yetu sasa wamelindwa rasmi kwa uamuzi wa Mahakama,”Zitto Kabwe.

Hata hivyo, amesema Mahakama imekataa kukubali maombi ya kuteuliwa kwa CAG mwingine kuwa ilikuwa batili.

“Hili tutakwenda Mahakama ya Rufaa ili iweze kulitolea maamuzi. Kama kuondolewa kwa Prof Assad ilikuwa batili ni dhahiri kuwa kuteuliwa kwa mtu mwengine kushika nafasi hiyo ilikuwa batili pia. Nimeshatoa maelekezo kwa mawakili wangu wakate Rufaa katika eneo hilo la hukumu.

“Nachukua nafasi hii kuwashukuru sana mawakili wangu Rugemeleza Nshala na Nyaronyo Kicheere kwa kazi kubwa ya kuniwakilisha. Vile vile wakili Bonifasia Mapunda ambaye alikuwa wakili wa Prof. Assad katika Kesi hii,” amesema.

Itakumbukwa kuwa Novemba 3, 2019,Rais Magufuli wakati huo akiwa madarakani alimteua Mkaguzi Mkuu mpya, Charles Kichere kuchukua nafasi ya Profesa Mussa Juma Assad.

Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Taarifa ya ikulu ilieleza kuwa kipindi chake Profesa Assad cha miaka 5 katika nafasi hiyo kilishia tarehe hiyo 3, Novemba, 2019 saa sita usiku.

Akizungumza baada ya kumuapisha CAG mpya, Rais Magufuli alimkumbusha CAG mpya kwamba yeye si muhimili wa serikali bali ni mtumishi tu.

Wakati Profesa Assad aliviambia vyombo vya habari ingekuwa bora watu wengine wakafafanua juu ya uamuzi huo kwani ni hatua ya kisheria, kwa kuwa suala hilo linafungamana naye.

“Jambo hili si la kisiasa ni jambo la kisheria, lakini nasema riziki anayo mwenyewe Mwenyezi Mungu…, kuna vitu chungu nzima za kufanya Inshallaah, Mungu atatufanyia wepesi na kila kitu kitakwenda vizuri,” alieleza Profesa Assad.

CAG Assad akiwa madarakani aliingia katika mgogoro mkubwa na Bunge kwa kile Spika wa wakati huo, Job Ndugai alichokiita kulidharau bunge hilo kwa kuliambia ni dhaifu na hivyo bunge kupitisha azimio la kukataa kufanya kazi na Profesa Assad.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!