July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama: Hatukusimamisha uchaguzi wa Meya

Spread the love

MGOGORO wa uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam umeingia katika sura mpya baada ya Mahakama kukana kutoa amri ya zuio la kufanyika kwa uchaguzi huo, anaandika Regina Mkonde.

Uchaguzi huo uliahirishwa kufanyika juzi Jumamosi baada ya Sara Yohana, Mkurugenzi wa Jiji, kuwasomea wajumbe wa mkutano wa uchaguzi kile alichodai ni “amri ya zuio la kutofanyika uchaguzi” ambayo alidai ilitokana na shauri lililofunguliwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Shauri lenye Na. 34 la 2016, lilifunguliwa Februari 5, 2016 na Susan Ernest Massawe na Saad Mohamed Khimji kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini mahakama imesema shauri hilo lilifutwa Februari 23 baada ya waliolifungua kushindwa kufika mahakamani siku iliyokuwa lisikilizwe.

Kutolewa kwa taarifa hizi na Mahakama kunakuja sambamba na kuwepo uvumi kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata wabunge na madiwani kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kati ya wabunge hao, alitajwa Saed Kubenea, mbunge wa Jimbo la Ubungo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL).

Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alikaririwa na ITV jioni leo akisema Kubenea pamoja na Halima Mdee (Kawe) wameshikiliwa kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Akizungumza na MwanaHALISI Online muda mfupi uliopita, Kubenea amesema hana tatizo na Polisi ndio maana alishirikiana nao kutoa maelezo yaliyohusiana na Mahakama kusema haijasimamisha uchaguzi wa Meya kwa sababu hakuna kesi inayohusu uchaguzi huo.

“Nilifika kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumjulisha hizi taarifa tulizothibitishiwa na Mahakama ya Kisutu kwamba kesi iliyodaiwa kufunguliwa na wajumbe wa CCM na kutolewa amri ya zuio la uchaguzi, si ya kweli. Kuna wahalifu waliokula njama ili kuvuruga uchaguzi halali wa Meya,” amesema.

Kubenea amesema Polisi wameahidi kuwa watafuatilia taarifa hizo na kuwakamata haraka iwezekanavyo wale wote waliohusika na kusababisha vurugu kwa kuitumia mahakama.

Kubenea amesema walipata taarifa hizo walipokwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia shauri kwa lengo la baadhi ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa Meya kujiunga katika shauri hilo lililodaiwa kufunguliwa na Massawe na Khimji ambayo ilitumika kupata zuio la uchaguzi.

Hata hivyo walivyoelezwa na maafisa wa Mahakama ya Kisutu ni kwamba hakuna zuio lilitolewa na kwamba hakuna kesi yoyote kwenye mahakama hiyo inayohusiana na uchaguzi wa Meya wa Jiji la dar es Salaam.

Taarifa zilizopatikana muda huu zimesema mbunge wa Kawe na maofisa wawili wa Chadema wamepelekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Kanda Maalum baada ya kutoa maelezo jioni.

error: Content is protected !!