August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahaba ya Jecha kwa Dk. Shein yatimia

Spread the love

KILELE cha mahaba ya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yametimia baada ya kumtunuku Dk. Ali Mohammed asilimia 91 ya ushindi, anaandika Happyness Lidwino.

Dk. Shein leo ametangazwa na ZEC kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika visiwani Zanzibar baada ya ule wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana kufutwa kinyume cha sheria.

Uchaguzi huo umefanyika jana huku kukiwa na hali ya wasiwasi kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) kuendelea na msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi huo.

Kabla na baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Zanzibar imepoa, hakuna shamra wala nderemo isipokuwa kwenye maeneo ambayo vikundi vidogo vilijikusanya na kuanza kupiga yowe.

Jecha amemtangaza Dk. Shein (CCM) kuwa ndiye mshindi wa kwanza kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.

Akitangaza matokeo hayo, Jecha amemtangaza Hamad Rashid Mohamed (ADC) kushika nafasi ya pili kwa kura 9,734 sawa na asilimia 3.0.

Awali Hamadi alidai kwamba, kutokana na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea urais wa CUF kususia uchaguzi, angeweza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) endapo angefikisha asilimia 5 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Kutokana na kushindwa kufikisha asilima 5 kwenye uchaguzi huo, Hamad ambaye alifukuzwa na CUF kutokana na tuhuma za usaliti katika chama hicho, ndoto zake zimefeli.

Jecha amemtangaza Maalim Seif (CUF) kupata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9 ambapo amedai kwamba, wapiga kura walikuwa 503,580 ambapo jumla ya kura zilikuwa 341,885 sawa na asilimia 7.9 huku kura zilizoharibika ni 13,538 sawa na asilimia 4.0 na kura halali zilikuwa 328,327 sawa na asilimia 96.0.

Majimbo mbayo Shein amepata kura nyingi ni pamoja na Chonga kura 3598, Chake chake 4551, Ziwani 2890 na Ole kura 3818.

Matokeo hayo yametangazwa leo ikiwa baada ya saa 30 tangu kupigwa kwa kura, ambapo leo matokeo yametangazwa katika Ukumbi wa Salama Hall   Bwawani ambapo watu mbalimbali walihudhulia wakiwemo waangalizi wa ndani ambao pia walionekana kutokuwa na shamra shamra na matokeo hayo.

Hata hivyo matokeo hayo pia yametangazwa huku baadhi ya wagombea kutokuwepo ndani ya ukumbi huo jambo ambalo limeibua maswali mengi kwa wananchi.

Hata hivyo, utangazwaji wa matokeo hayo umewashangaza wengi kutokana na kutokuwepo kwa mawakala wa vyama vingine isipokuwa CCM pekee.

Imebainika kuwepo kwa wanaojiita wasimamizi kwenye uchaguzi huo lakini pale walipoulizwa chama wanachokiwakilisha, alishindwa kutaka anachokiwakilisha.

error: Content is protected !!