September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magwiji wa vyeti ‘feki’ wapandishwa kizimbani

Spread the love

WATU watatu wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini  Dar es Salaam wakikabiliwa kwa tuhuma za kughushi vyeti na nyaraka mbalimbali, anaandika Faki Sosi.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 132 ya kughushi nyaraka, vyeti na mihuri mbalimbali.

Mwamba Mwamba (38)  mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), Mahundi Zubeir (24) mwanafunzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (VETA) na Ashraf Maumba ambaye ni mfanyabiashara ndiyo wanaokabiliwa na mashitaka hayo.

akisoma mashitaka yao, Nassoro Katuga, wakili wa serikali mbele ya Respicius Mwijage Hakimu Mkazi katika Mahakama hiyo amedai kuwa katika shtaka la kwanza watuhumiwa wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa.

Katuga amedai kuwa watuhumiwa katika tarehe isiyofahamika maeneo ya Buguruni Dar es Salaam watuhumiwa kwa pamoja walikamatwa wakijihusisha na utengenezaji wa vyeti na mihuri ya bandia.

Katuga amedai kwamba watuhumiwa hao walitengeneza jumla ya vyeti 60 kwa kutumia jina la Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na kwamba katika vyeti hivyo kipo chenye namba ACS 0359955 cha mtu anayefahamika kama Abdulla Mohamed Noor.

Wakili huyo ametaja vyeti vingine walivyoghushi katika mashtaka
hayo kuwa ni pamoja na cheti kimoja kutoka Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) kilichotolewa Novemba 2009, kingine kimoja kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Katuga amedai mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa pia wanakabiliwa na mashitaka ya kughushi mihuri mbalimbali ya ofisi za Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Chuo cha Mamlaka ya Bandari, VETA na mingine mingi kutoka katika ofisi mbalimbali za umma.

Mashtaka mengine ni kukutwa na jumla ya kadi 53 za magari ambazo zinaonesha ni halali kutoka katika ofisi ya TRA, kukutwa na vyeti Saba kutoka kwa Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Katuga akiongoza jopo la mawakili wa serikali ameiomba mahakama kuwapa masharti magumu watuhumiwa  kupitia kifungu cha 148 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, kutokana na kutokamilika kwa upelelezi wa shauri hilo na unyeti wa makosa yao.

“Tunaomba watuhumiwa wapewe masharti mazito suala la kughushi limehusisha ofisi nyeti za serikali na tunaomba wasipewe dhamana kwa kuwa watakapotoka wanaweza kuathiri ushahidi na upelelezi wa unaoendelea kwa sasa,” amedai Katuga.

Hakimu Mwijage amesema Mahakama imekubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuwapa muda wa mwezi mmoja ili kukamilisha taratibu za
upelelelezi ili watuhumiwa waweze kudhaminiwa.

Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi 11 Agosti mwaka huu kwa ajili ya watuhumiwa kuanza kusomewa maelezo ya awali.

 

error: Content is protected !!