MAMIA ya magunia ya madawa ya kulevya aina ya bangi, yamekamatwa wilayani Arumeru mkoani Arusha, mchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Haya yanatokea kufuatia operesheni kambambe ya kukamata, kuharibu dawa aina ya bangi, inayofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).
Aidha, takribani hekari 308 za mashamba ya bangi, yameteketezwa wilayani humo katika operesheni hiyo.
Operesheni ya kuteketeza mazao hayo, imefanyika jana, tarehe 1 Juni mwaka huu, katika kijiji cha Lesinoni, ambako jumla ya gunia 249 ya bangi kavu zikikamatw na hekari 207 za mashamba ya bangi zikiteketezwa.
Katika operesheni iliyofanyika, tarehe 31 Mei 2023, katika kijiji cha Kisimiri Juu, DCEA ilikamata gunia 482 za bangi na kuteketeza hekari 101 za mashamba ya zao hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishena Jenerali Aretas Lyimo, leo 2 Juni 2023, watuhumiwa tisa wamekamatwa katika operesheni hiyo, wakihusishwa na matukio hayo.
Akisitiza idara yake kuendelea na operesheni za aina hiyo, Kamishena Jenerali Lyimo amesema: “Mamlaka ya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara maeneo yote nchini.”
Alisema, “lengo ni kuhakikisha kilimo cha bangi na mirungi kinatokomezwa kabisa na wananchi wanajikita katika kilimo cha mazao mbadala ya biashara na chakula.”
Taarifa ya serikali kuhusiana na dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, inaitaja mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara, kuwa vinara wa kilimo cha bangi.
Leave a comment