September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli: wakosoaji acheni viherehere

Spread the love

RAIS John Magufuli amewataka wanaozikosoa ndege mbili mpya aina ya Bombardier Dash-8 Q400 zilizonunuliwa na serikali ya Tanzania hivi karibuni kuacha viherere, anaandika Charles William.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika tukio la uzinduzi wa ndege hizo, lilifanyika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK. Nyerere.

“Mmezoea kusifia vya nje, wewe kama huzipendi si ukae kimya, kiherehere cha nini? Hizi ndege zitapandwa na watanzania wote, atapanda Mbowe (Freeman), atapanda Lipumba (Prof. Ibrahim) watapanda CCM na hata mtu akija na hirizi yake atapanda,” amesema.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewaonya wafanyakazi wa shirika la ndege la ATCL na kuwataka wajipime kama wanaweza kufanya kazi kwa kasi inayohitajika au la.

“Wale wanaotaka kufanya kazi na ATCL wajisahihishe, waseme wametubu, wameokoka na wanataka kufanya kazi ya watanzania. Hatuoni hasara kupunguza wafanyakazi, tulipunguza wafanyakazi 500 wa NIDA (Mamlaka ya vitambulisho vya taifa), tutashindwa hawa 200?” Amehoji.

Rais Magufuli ametaja kile alichokiita dhambi za shirika la ndege la ATCL katika kipindi cha nyuma na kuionya bodi ya shirika hilo kutorudia makosa hayo kwani serikali haitayafumbia macho.

“ATCL ilikuwa haijiendeshi kibiashara, ilikuwa ikitegemea serikali mpaka katika kulipa mishahara ya serikali. Kulikuwa na mafuta hewa ya ndege ambapo ndege inadaiwa kuwa imeruka kutoka Dar mpaka Mwanza na mafufa yametumika wakati ipo hapahapa Dar.

“ziliwahi kupotea milioni 700 katika kituo cha Comoro na aliyehusika na upotevu huo baada ya kustaafu mwezi wa pili mwaka huu ameongezewa mkataba ili azidi kupoteza fedha zaidi,” ameeleza Rais Magufuli.

Akielezea mipango ya serikali kulikuza zaidi shirika hilo, Rais Magufuli amesema serikali yake ina mpango wa kununua ndege mbili kubwa na kwamba fedha tayari zipo ambapo ndege moja miongoni mwa zitakazonunuliwa itabeba watu 160 nyingine itabeba watu 240.

Amegusia pia juu ya uwepo wa wafanyakazi wa ATCL ambao ni wake wa mawaziri wa serikali, na kuhoji inawezekana vipi waziri akubali mke wake afanye kazi katika shirika ambalo halizalishi, huku akisema hakuna mtu atakayeruhusiwa kupanda ndege hizo bila kulipa.

“Msiruhusu mtu kusafiri bure hata kama ni kiongozi wa serikali, kwasababu mna tabia ya kujipendekeza. Hata nikipanda mimi mnitoze, akiingia Waziri Mkuu atozwe na hata akipanda waziri Mbarawa naye mmtoze kwelikweli. Hiyo ndiyo maana ya biashara,” amesema.

error: Content is protected !!