RAIS wa Tanzania, John Magufuli amesema, Serikali anayoiongoza itaendelea kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 13 Novemba 2020 wakati akihutubia na kufungua Bunge la 12 jijini Dodoma.
Ameanza hotuba yake kwa kutoa shukurani kwa uongozi wa Bunge ukiongozwa na Spika Job Ndugai kwa kuchaguliwa na wabunge kuendelea kuwa Spika wa Bunge hilo kwa miaka mitano mingine “hongera sana.”
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amechaguliwa kuwa Spika kwa Bunge hilo la 12 akiendelea na nafasi hiyo aliyokuwa nayo Bunge lililopita la 11.
“Nampongeza pia Dk. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa Naibu Spika; tena mara hii akiwa Mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Mbeya Mjini.”

“Hongera sana Dk. Tulia. Huu ni uthibitisho kwamba, nchi yetu, kupitia Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, inawaamini sana wanawake,” amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wabunge.
Rais Magufuli amesema, “kama mnavyofahamu, Makamu wetu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, naye ni mwanamama. Aidha, Bunge hili la 12 nalo lina wabunge wengi wanawake.”
“Kwa msingi huo, napenda nitumie fursa hii kuahidi kuwa, Serikali ninayoingoza, itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Wanawake na akinamama Oyee!!!,” amesema Rais Magufuli na kuibua shangwe bungeni.

Pia, Rais Magufuli amewapongeza wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hilo la 12.
“Mmechaguliwa kwa vile wananchi wana imani kuwa mna uwezo wa kuwawakilisha vizuri. Hivyo basi, nawasihi msiwaangushe wananchi waliowachagua. Watanzania wana imani kubwa sana na Bunge hili,” amesema Rais Magufuli.
Leave a comment