MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli amesema, Serikali anayoingoza, imefanya mambo makubwa kwa wananchi huku akitamani kuifanya nchi hiyo kuwa kama Ulaya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea)
Dk. Magufuli ambaye ni Rais wa Tanzania, amesema hayo leo Alhamisi tarehe 6 Agosti 2020 makao makuu ya chama hicho Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini humo alikokabidhiwa fomu za kuwani urais.
Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa wa madiwani, wabunge na Rais Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Rais Magufuli amesema, walipochaguliwa kuongoza Taifa hilo kwa awamu ya tano na kupeperusha bendera ya CCM, yapo mengi tumeyafanya, ni mengi sana, yanahitaji siku, mwezi na mwaka kuyaeleza yote
“Kila mahali katika nchi hii, pamefanyika kitu, kila mahali, kila tulipogusa, shule za msigi zilizojengwa zaidi ya 908, shule za sekondari zaidi ya 228, vituo vya afya karibu 500.”
“Wakati tunaingia madarakani, nchi yetu ilikuwa na vijiji 3,000 tu vilikuwa na umeme lakini sasa vimefika 9,402 na tumebakisha vijiji kama 3,000 kumaliza vyote. Sasa tukipewa miaka mitano tena tushindwe kumaliza vijiji hivyo. Ni mengi mno yamefanyika,” amesema
Rais Magufuli amesema, wamejitahidi kuthibiti utoroshaji wa madini na kutungwa kwa sheria nzuri na Bunge la Tanzania chini ya Spika Job Ndugai zinazosimamia rasilimali za Taifa.
“Spika nitashangaa sana Bunge linalokuja waache kukuchagua wewe kuwa Spika, watasema nakupigia kampeni, nina haki ya kukupigia kampeni, aliunda Tume ya Madini kwenda kuchunguza na tukabadilisha sheria na hiyo sheria ni the best kwenye nchi hii,” amesema Rais Magufuli
“Tanzania ni Taifa tajiri, lakini tulikuwa tumezoeshwa kuambiwa ni masikini na ndiyo maana Tanzania imeingia uchumi wa kati, ni nchi chache Afrika zimeingia uchumi wa kati ni Tanzania, Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Togo na zingine chache. Kwa nini tumeingia uchumi wa kati, tumeimiliki vizuri rasilimali zetu,” amesema
Huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema “nataka Tanzania iwe kama Ulaya, nataka nchi hii iwe kama Ulaya, sisi ndiyo tuwe tunatoa misaada na uwezo tunao na kikubwa ni mipango na mipango imetengezwa na chama changu cha mapinduzi.”
Leave a comment