August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli: Nakuja, CCM mjiandae

Spread the love

RAIS wa awamu ya tano wa Tanzania ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewataka wanachama wa chama hicho kujiandaa kwa mabadiliko makubwa, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa CCM, Magufuli ameahidi kuunda safu bora ya uongozi ndani ya chama hicho huku akijipanga kufumua katiba ya CCM na kuondoa vyeo vyote visivyo na tija kwa wakati huu.

“Vipo vyeo vingi ndani ya chama visivyo na tija, kwa sasa tuna watoto chipukizi wenye miaka nane mpaka 15. Kama patakuwepo watoto chipukizi wa CCM, wakianzishwa chipukizi wa Chadema au UDP na vyama vingine hawa watoto watasoma saa ngapi?” amehoji Magufuli.

Magufuli pia amehoji uwepo wa makamanda wa jumuiya mbalimbali za CCM kwa kusema; “Je bado kuna umuhimu wa kuwa na makamanda wa chama ambao wana pesa pekee? vyeo hivi vinasaidia utatuzi wa matatizo ya wananchi au vinaongeza migogoro wakati wa uchaguzi?”

Katika hatua nyingine Magufuli amesema kitendo cha wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kuimba jina la Edward Lowassa mwaka jana baada ya chama kumkata kilikuwa cha kuudhi na angekuwa mwenyekiti wa CCM angechukua hatua kali dhidi ya wajumbe husika.

“Nakumbuka siku tuliyoingia kwenye mkutano halafu zikasikika sauti za wajumbe wakiimba jina la mtu fulani, ningekuwa mimi ndiyo mwenyekiti robo au nusu ya wajumbe hao wangepotea,” amesema Magufuli na kuongeza,

“Najaribu kuuliza moyo wangu, kingetokea kwangu kilichotokea kwako, lakini wewe ulivumilia, ukawahusisha wazee na mambo yakawa mazuri, umetoa fundisho zuri kwetu kwamba siku nyingine uvumilivu ni jambo zuri katika uongozi.”

Magufuli amesema kuwa hana uhakika hatakuwa na uvumilivu kama wa Kikwete hata hivyo ameomba wanachama wa chama hicho wamuombee kwa Mungu ili apate japo nusu ya uvumilivu wa wa mtangulizi wake na kusudi mambo yetu yaende salama.

Pamoja na mengineyo pia mwenyekiti huyo mpya wa CCM ameahidi kuzingatia maslahi ya watumishi wa chama hicho na kusema hatapenda kuona watumishi wa chama hicho wakigeuka omba omba kutokana na maslahi duni.

error: Content is protected !!