August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli na serikali vipande

Spread the love

BAADA ya kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwa mshindi wa kiti cha urais na baadaye kuapishwa, Rais John Magufuli aliahidi kuunda baraza dogo la mawaziri, anaandika Saed Kubenea.

Alisema baraza lake litakuwa imara na litakidhi matakwa ya wananchi; na kwamba litasheheni waadilifu na wachapakazi.

Lakini baada ya kujifungia Ikulu kwa zaidi kidogo ya siku 30, akaja na baraza la mawaziri vipande-vipande.

Mawaziri wanne wa kuongoza wizara nyeti – wizara ya Fedha na Mipango; Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi; Ujenzi na Maliasili na Utalii – walikosekana.

Hadi sasa, rais hajaeleza nani aliyemlazimisha kutangaza baraza la mawaziri likiwa halijakamilika.

Alisema baraza aliloliteua lina mawaziri 19. Lakini wizara zilizotajwa zilikuwa 18. Hakufafanua.

Ndani ya baraza hilo, akajaza watuhumiwa wa ufisadi na wachovu. Baadhi ya walioteuliwa, ni wale waliokaribia kukizamisha chama chake kwa tuhuma mbalimbali.

Miongoni mwao ni Prof. Sospeter Muhongo. Bunge lilimtuhumu ufisadi kuhusiana na mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Tegeta Escrow. Magufuli amemrejesha katika wizara ileile – nishati na madini.

Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), katika ukurasa wa 58, inamtaja Prof. Muhongo kuwa ndiye aliyekuwa “dalali mkuu” aliyewakutanisha Bw. Harbinder Singh Sethi na Bw. James Rugemalira.

Sethi ndiye alijiita mmiliki mpya wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Rugemalila alikuwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa katika IPTL.

Ruhusa ya kuuza kampuni ya IPTL kwa mwekezaji mwingine; agizo kwa Tanesco kujifunga katika mkataba mwingine wa miaka mitano wa kununua umeme kwa mwekezaji mpya; yote haya yanatajwa kufahamika na kuhusishwa na Prof. Muhongo.

Prof. Muhongo anajua kuwa mkataba wa miaka 20 kati ya serikali na IPTL ulikuwa unakaribia kufika tamati; lakini akiwa waziri mhusika, ama aliruhusu, kubariki au kulazimisha Tanesco kujifunga katika mkataba mwingine.

Mkataba wa awali kati ya serikali na IPTL unaelekeza kuwa mara utakapofika kikomo, mitambo ya IPTL iliyoko Tegeta, Salasala, jijini Dar es Salaam, itakuwa mali ya Tanesco moja kwa moja.

Utiaji saini mkataba mpya wa miaka mitano, huku waziri Muhongo akiwepo na kushuhudia masharti ya mkataba wa awali yakivunjwa, ulilenga kuipora Tanesco haki ya kumiliki mitambo ya IPTL. Ndivyo ilivyo hadi leo.

Aidha, ndani ya Bunge, Prof. Muhongo alipatikana na hatia ya kuvunja kifungu cha 29 cha sheria ya fedha ya mwaka 2012.

Kifungu kinamtaka waziri husika, kuthibitisha uuzaji wa hisa, pale makampuni mawili au matatu yanapoamua kuuza hisa zao. Hakufanya hivyo. Mteule wa Magufuli.

Rais Magafuli hakuishia hapo. Alimteua Prof. Makame Mbarawa kuwa waziri wa Maji na Umwagiliaji. Siku tatu baadaye akamuondoa na kumfanya kuwa waziri wa ujenzi.

Prof. Mbalawa, raia kutoka nchi jirani –Tanzania Zanzibar – akakabidhiwa kuongoza wizara ya Tanganyika.

Naye Eliakim Maswi, mtuhumiwa mwingine katika sakata la Tegeta Escrow, akateuliwa kuwa Naibu Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Maswi alikuwa katibu mkuu wa nishati na madini.

Dk. Philip Mpango, akafanywa waziri wa Fedha na Mipango. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mpango alikuwa Kaimu Kamishina mkuu wa TRA. Alipelekwa huko kutokea Tume ya Mipango.

Lakini kali kuliko zote ni hili la Ijumaa iliyopita, ambapo Jenista Mhagama, waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alimtangaza Dk. Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Jenesta akafika mbali zaidi. Alimtambulisha mkurugenzi wake mpya kwa menejementi ya NSSF. Lakini uteuzi wa Wangwe ulifutwa saa tano tu baadaye. Wateule wa Magufuli.

Kikao cha menejementi ambacho mkurugenzi mpya alitambulishwa kilihudhuriwa pia na Antony Mavunde, naibu waziri wa wizara hiyo.

Baada ya kikao cha utambulisho, Dk. Wangwe alipata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi na kueleza mikakati yake.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilisema, “uteuzi wa Dk. Wangwe umefutwa kwa sababu ya baadhi ya taratibu kutokamilika.”

Dk. Wangwe aliteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya Rais Magufuli kumteua Dk. Ramadhan Dau kuwa balozi mwezi uliopita.

Kabla ya kufanywa kuwa kaimu mkurugenzi wa NSSF, Dk. Wangwe alikuwa mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari, Elimu na Mawasiliano (Tehama), katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Mhagama alisema, “…kwa mamlaka niliyopewa ya kusimamia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ninamteua Dk. Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF. Uteuzi unaanza 27 Februari na utakoma pale rais atakapoteua rasmi mkurugenzi mkuu wa shirika.”

Lakini taarifa ya Ikulu iliyotengua uteuzi wa Mhagama ilisema, kutenguliwa kwa uteuzi huo, kunatokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu.

Kwamba uteuzi mpya kwa mujibu wa mamlaka na sheria utakapofanyika, taarifa zitatolewa kwa wananchi.

Hadi sasa, siyo waziri Mhagama wala Ikulu iliyotoa maelezo yanayotosheleza kuhusu kufutwa kazi kwa Dk. Wangwe.

Kwa mfano, Balozi Sefue amenukuliwa akidai kuwapo kwa mwingiliano wa mawasiliano katika vyombo vya serikali. Hakuvitaja.

Alisema Dk. Wangwe alipaswa awe mwangalizi tu (Caretaker) wa shirika; siyo kaimu mkurugenzi; na kwamba neno la Kiswahili la “caretaker” lilikosewa na kuandikwa kaimu mkurugenzi mkuu.

Kauli ya Balozi Sefue, inalenga kuaminisha umma kuwa waziri Mhagama hafahamu maana ya neno Caretaker. Hafahamu tofauti kati ya kaimu mkurugenzi na mwangalizi wa shirika.

Hili linadhihirisha kuwa hakuna mawasiliano kati ya waziri anayetafuta mtu wa kuangalia shirika; na ofisi ya rais inayoteua mkurugenzi.

Kwamba serikali haina muunganiko wa pamoja. Inakurupuka. Inatenda kazi zake, mithiri ya mbolea ya mbuzi.

Ni kama vile inaendeshwa bila vikao na kufanyika maamuzi kwa kutumia kichwa kimoja.

Huo ndio uteuzi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Makala hii imeandikwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo namba 329 la tarehe 7 Machi 2016.

error: Content is protected !!