MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema, wananchi wa Tunduma, Mkoa wa Songwe wakichagua mgombea nje ya chama hicho, hatopeleka maji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tunduma … (endelea).
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi tarehe 1 Oktoba 2020 wakati akihutubia mkutano wa kampeni zake za urais katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Julius Kambarage Nyerere, Tunduma.
Amesema, sasa ni mara ya mwisho kuwaomba.
“…lakini msinichanganyie, mkiniletea hao nasema maji hamyapati. Lazima tuambizane ukweli na mimi nazungumzaga ukweli. Huwezi kupeleka chakula kwa jirani wakati mtoto wako ana njaa. Hata malaika wanachagua pa kwenda.”
“Huwezi watu unawabaembeleza kila siku. Miaka mitano iliyopita nilisimama kwenye uwanja nikawabembeleza, mkasema hapa na miaka mingine mkasema hapana. Hii ni mara ya mwisho mimi kuwaomba, siwatishi lakini ninasema ukweli,” amesema Dk. Magufuli.

“Nimevumilia moyo mpaka unauma, mnataka niwaletee mpaka malaika? Hata Sodoma na Gomora Mungu alipowapelekea malaika, alivumilia mpaka akashindwa,” amesema
Dk. Magufuli amewataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua David Silinde, mgombea ubunge wa kupitia CCM na kwamba, anamujua vizuri mgombea huyo na ndio maana alimpitisha kugombea ubunge licha kwamba kwenye kura za maoni hakuongoza.
“Mimi ni Mwenyekiti wa CCM, nisingempitisha huyu aliyekuwa Chadema, ninafahamu matunda yake na uzuri wake… hata CCM wapo waliokuwa wanampiga vita, hata Chadema alipotoka wapo wanaompiga vita.”
“Nileteeni Silinde halafu mje mniulize maji ya hapa…na ukweli nimeishaanza kuipanga hiyo miradi. Tunataka tuyatoe maji Ileje yateremke kwa mmiminika mpaka hapa Tunduma, mtakunywa mpaka mtachoka,” amesema.
Mgombea huyo amesema, kiasi cha Sh.2.579 bilioni zilitolewa kwa ajili ya miradi ya maji lakini mpaka sasa hakuna maji.
Amewataka wananchi wa jimbo hilo kumuuliza yule waliyemchagua kuhusu miradi ya maji kwa kuwa yeye hawezi kuwauliza.
“Ndio maana nasimama hapa kuwaomba ndugu zangu wa Tunduma, mniletee madiwani wa CCM, mniletee wabunge wa CCM ili kusudi pesa zitakapopotea, nijue namna ya kuwahoji, wale wengine siwezi kuwahoji, mkitakiwa nyinyi muwahoji. Sasa mniletee hawa ili niwahoji mmi mwenyewe,” amesema.
Frank Mwakajoka kutoka Chadema, ndiye aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake ambaye pia, anagombea tena jimbo hilo akichuana na Mwakajoka.
Leave a comment