January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli mgeni rasmi Kagame Cup

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akimtangaza John Magufuli kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi na mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kagame siku ya Jumamosi, Julai 18 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Magufuli baada ya kufungua rasmi michuano hiyo, atashuhudia mchezo wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya Kagame, mechi itakayowakutanisha miamba ya Afrika Mashariki timu ya Yanga dhidi ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya. 

Michuano ya Kagame inatarajiwa kuanza kutimua vumbi siku ya Jumamosi kwa michezo mitatu, ukiondoa mechi ya Yanga na Gor Mahia, mechi zingine zitakua ni kati ya APR dhidi ya Al Shandy uwanja wa Taifa saa 8 mchana, KMKM Vs Telecom saa 10 jioni uwanja wa Karume.

Mchezo wa ufunguzi  kati ya Yanga dhidi ya Gor Mahia unaonekana kuteka hisia za wapenzi wa soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kwani ni takribani miaka 19 timu hizo mbili haziwaji kukutana katika ardhi ya Tanzania. 

Mara ya mwisho mwaka 1996 katika michuano ya Cecafa, timu hizo zilikuwa katika kundi moja, katika mchezo wa awali zilitoka sare ya bao 1- 1, wakati zilipokutana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Gor Mahia iliibuka na ushindi wa mabao 4 -0. 

Gumzo la wadau wa soka nchini kwa sasa ni kuhusu uwezo wa klabu za Tanzania, Yanga, Azam na KMKM kuweza kuhakikisha kombe la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki haliondoki kwenye ardhi ya nyumbani.

error: Content is protected !!