January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli: Lipeni urais Tingatinga

Spread the love

MGOMBEA wa Urais wa CCM Dk. John Magufuli amejinadi kuwa anaomba Urais kwa kuwa yeye ni ‘tingatinga’ linaloweza kuleta maendeleo kwa watanzania kwa kasi inayohitajika. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama hicho katika uwanja wa Mpilipili mjini Lindi, Magufuli ameitetea Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa imefanya mambo mengi mazuri ndani ya utawala wake wa miaka 54 tangu uhuru hivyo ni vyema ikaendelea kupewa nafasi.

Magufuli pia ameonyesha matamanio yake katika nafasi hiyo ya juu zaidi ya kisiasa hapa nchini kwa kusema “Nilikua natumwa na maraisi wangu, naomba mnipe nafasi na mimi nikatume.”.

Mgombea huyo amewaita wale wanaoipinga CCM na Kusema serikali hiyo haijafanya kitu chochote kuwa ni waongo na wenye ‘shukrani za punda’.

“Ndugu zangu Lindi hii haikuwa hivi miaka ya nyuma, sasa hivi kuna lami na barabara zinazopitika kiurahisi na hii yote ni kazi nzuri ya serikali ya CCM ndio maana tunaomba mkiamini tena ili kiweze kuendelea pale kilipoishia” alisisitiza.

Katika hatua nyingine aliyekuwa miongoni mwa wagombea Urais wa chama hicho Benard Membe amewataka watanzania kupuuza uvumi kuwa aliyekuwa Gavana wa benki kuu ya Tanzania BOT, Daudi Balali bado yupo hai na kusema hizo ni propaganda.

Membe anasema kuwa “Nimesikia Lowassa anasema atamfufua Balali iwapo atachaguliwa kuwa Rais, mimi nasema Balali amekufa anayetaka kumrudisha tena mwambieni yeye sio Yesu, Ni Yesu pekee ndio alimfufua Lazaro”

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na katibu wa halmashauri kuu ya chama hicho NEC, itikadi na uenezi Nape Nauye pamoja na mke wa Rais Kikwete mama Salma huku wote wakiwataka wakazi wa Lindi mjini kuendelea kukiamini chama hicho kwa kukichagua tena.

Katika mkutano huo wasemaji mbalimbali wa chama hicho waliwashambulia makada mbalimbali walioihama CCM na kujiunga na vyama vya upinzani wakiwataja kama ‘wasaliti’ kwa chama hicho.

Miongoni mwa wanasiasa wakongwe waliohamia vyama vya upinzani mwaka huu wakitokea CCM ni Mgombea Urais wa Chadema Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye pamoja na aliyekuwa kada wa chama hicho tangu kuzaliwa kwa TANU, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye hajajiunga na chama chochote lakini anashiriki kampeni za Urais za Ukawa.

error: Content is protected !!