December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli kuhutubia Bunge Ijumaa

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli atalizindua Bunge la 12 Ijumaa tarehe 13 Novemba 2020 sa 3:00 asubuhi jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Akiahirisha shughuli za Bunge leo asubuhi Jumatano tarehe 11 Novemba 2020 jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, siku hiyo Rais Magufuli ataweka wazi dira ya Serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kama huu wa kwetu, huwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anahutubia Bunge kwa maana ya kuweka dira ya serikali yake kwa miaka mitano inayokuja na utekelezaji wa ilani kadri anavyoona inafaa.”

“Hotuba hiyo ni muhimu, anahutubia Bunge na taifa siku ya Ijumaa saa tatu kamili asubuhi,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema, kabla ya Rais Magufuli kuhutubia mhimili huo, kutakuwa na gwaride, pia wageni wengi wanatarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo.

Job Ndugai, Spika wa Bunge la 12 la Tanzania

“Niwataarifuni kwamba, kesho kutwa siku ya Ijumaa asubuhi saa tatu kamili nawaomba wabunge wote tuwe ndani na maelekezo mengine tutapata. Siku hiyo kutakuwa na gwaride na wageni wengi tunaomba tuwahi kufika tuwasili saa 2:00 asubuhi,” amesema Spika Ndugai.

Rais Magufuli atahutubia Bunge hilo siku chache kupita baada ya kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020 kuongoza Taifa hilo katika muhula wa pili wa miaka mitano na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Shughuli za Bunge jipya za kikao cha kwanza, zilianza jana Jumanne ambapo kulifanyika uchaguzi wa Spika ambapo Job Ndugai alishinda akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.

Baada ya kushinda na kuapishwa, alianza kuwaapisha wabunge wateule.

error: Content is protected !!