May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli kuhamishia sherehe za Uhuru Dodoma

John Magufuli, Rais wa Tanzania akihutubia katika sherehe za miaka 55 ya Uhuru

Spread the love

RAIS John Magufuli amesema sherehe za kumbukumbu ya siku ya Uhuru zilizofanyika leo ndizo za mwisho kufanyika jijini Dar es Salaam kwani tarehe 9 Desemba mwakani zitahamishiwa makao makuu ya nchi, mkoani Dodoma, anaandika Pendo Omary.

Rais Magufuli pia ameeleza sababu za kufuta sherehe hizo mwaka jana ambapo amesema gharama kubwa za sherehe hizo pamoja na kutokamilika kwa uundaji wa serikali ikiwa ni muda mfupi tangu kuingia madarakani ilikuwa ni miongoni mwa sababu hizo.

“Mwaka jana niliamua tuadhimishe sherehe za Uhuru kwa kufanya usafi kwa sababu sherehe hizo zilitakiwa kufanyika mwezi mmoja baada ya mimi kuingia madarakani, nilikuwa sijakamilisha hata uteuzi wa Baraza la Mawaziri pamoja na watendaji wengine.

Lakini pia nilipouliza gharama zake nikaambiwa ni Sh. 4 bilioni ambazo niliagiza zitumike katika upanuzi wa barabara ya Ali Hassan Mwinyi ili kupunguza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam,” amesema.

Rais Magufuli amesema gharama za sherehe hizo kwa mwaka huu zimepunguzwa sana ingawa hakuweza kutaja kiasi halisi kilichopungua tofauti na bajeti ya miaka iliyopita, ambapo alidokeza kuwa katika sherehe za mwaka huu hakutakuwa na hafla ya chakula kwa wageni waalikwa.

“Mwaka huu hakutakuwa na chakula baada ya sherehe hizi, hakutakuwa na dhifa ya kitaifa. Shughuli ikimalizika hapa uwanjani kila mtu anaenda nyumbani kwake,” amesema.

Kabla ya kuanza kutoa hotuba yake Rais Magufuli alikagua gwaride la vikosi vya kijeshi sambamba na kupigiwa mizinga 21 huku pia akishuhudia burudani ya vikundi vya ngoma, kwaya na sarakasi.

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru ambapo zilihudhuriwa na wananchi mbalimbali, viongozi wa serikali wa sasa pamoja na wastaafu pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali. Zilianza rasmi saa 3:45 asubuhi na kumalizika 7:20 mchana.

error: Content is protected !!