July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli aweka jiwe la msingi Arusha

Spread the love

RAIS Pombe Magufuli amesema, hakutakuwa na sababu ya yeye kuitwa rais kama atashindwa kuwasaidia wananchi wa Tanzania kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, anaandika Hamisi Mguta.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati wa uwekwaji wa jiwe la msingi katika barabara yenye urefu wa Kilomita 234.3 inayotoka Tengeru mkoani Arusha kwenda Kenya.

Akizungumza na wananchi mkoani leo Arusha wakati wa uzinduzi huo Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema, wananchi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla ni jukumu lao kufaidika na umoja huo ambapo ndio lengo la kuundwa kwake.

Amesema, barabara inayojengwa mkoani humo ili kuunganisha mawasiliano ya nchi za Afrika Mashariki, inalengo kuongeza fursa ya kujiendeleza kibiashara na kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika Nchi za Afrika Mashariki.

“Kwa mara ya kwanza Arusha sasa itakua na barabara yenye njia nne na haya ndio maendeleo, Watanzania wa Arusha, Watanzania wa Afrika Mashariki ni ukweli watu hawahitaji mambo ya vyama vyama, wanataka maendeleo,” amesema.

Barabara hiyo kwa upande wa Tanzania ina urefu wa Kilomita 56.4 ambapo Kilomita 14.1 kutoka Arusha hadi Tengeru.

Rais Magufuli amesema, jumla ya Sh. 209.3 Bilioni zitatumika kujenga barabara hiyo, Sh. 190 Bilioni zimetolewa na African Development Bank na Jaica Shirika lililopo chini ya Serikali ya Japan na Sh. 19.4 Bilioni zimetolewa na Serikali ya Tanzania kushirikiana na East Africa Community.

“Nchi zilizo ndani ya Afrika Mashariki ni tajiri, hatutakiwi kuwa masikini kiasi hiki ni lazima tufike mahali tujiulize ni nani aliyeturoga, tumuombee asiroge tena,” amesema.

Rais Magufuli amesema, kutokana na asilimia 93.7 ya mizigo nchini Tanzania inasafirishwa kwa njia ya barabara hivyo barabara hiyo itasaidia kiasi kikubwa katika usafirishaji ndani ya nchi za Afrika Mashariki.

“Lazima nchi zote za Afrika Mashariki ziwe na barabara zinzopitika ili kujenga uhusiano wa karibu kibiashara,” amesema.

Akitoa maoni yake kupitia Kituo cha Radio cha Taifa kilichokua kikirusha matangazo ya moja kwa moja ya mkutano huo, Damas Mbuya, Mkazi wa Tengeru mkoani Mwanza amesema, hutuba zilizozungumzwa na marais kuhusu barabara hiyo ni za kimaendeleo na umuhimu wa barabara hiyo ni mkubwa.

Mbuya ametoa pongezi pia kwa Rais Magufuli kwa kuondokana pamoja na kusisitiza suala la kuweka kando uchama ili kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo.

error: Content is protected !!