August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli ‘awazima’ wanafunzi wajawazito

Rais John Magufuli

Spread the love

Rais John Magufuli amesema anaunga mkono hoja ya Mama Salma Kikwete, Mbunge wa kuteuliwa na Rais kuhusu Serikali kutoruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua, anaandika Charles William.

Mama Salma ambaye ni mke wa Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, akichangia bungeni, tarehe 15 Mei, 2017 alisema suala la wanafunzi wa sekondari na msingi kurejea masomo halikubaliki kwani ni kinyume na maadili ya kitanzania pamoja na misingi ya dini.

“Mimi sikubaliani na suala la wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni. Mila, desturi, utamaduni, mazingira na dini haziruhusu na hata Biblia na Quran zinakataza,” alisema Mama Salma na kuzua mjadala mkali ambapo wabunge mbelimbali akiwemo Suzan Lymo, walimpinga.

Suzan Lymo ambaye ni waziri kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alisema wanafunzi hawatakiwa kunyimwa haki ya kupata elimu baada ya kujifungua kwani, wapo wanafunzi ambao hupata ujauzito kwa kubakwa au kulaghaiwa na watu wazima na si sahihi kuwanyima kabisa fursa ya elimu.

Leo Rais Magufuli akizungumza katika mkutano wa hadhara wakati wa uzinduzi wa barabara ya Msata – Bagamoyo amesema hawezi kusikiliza asasi za kiraia zinazotaka kuliharibu Taifa.

Amempongeza Mama Salma kutokana na mchango wake alioutoa bungeni na kusema msimamo wake ulikuwa sahihi na thabiti.

“Mtu amezaa, iwe kwa makusudi, kwa bahati mbaya au kwa raha zake halafu azae arudi shuleni? Ndani ya utawala wangu kama Rais hakuna mtu mwenye mtoto katika elimu ya msingi na sekondari atakayerudi shuleni.

“Natoa elimu bure toka shule ya msingi mpaka sekondari halafu nisomeshe wazazi? Mzazi ni marufuku kurudi shule. Atafute elimu mbadala.

“Mwisho utakuta darasa la kwanza wote wanawahi kunyonyesha, kwasababu mchezo huo ni mzuri na kila mmoja angependa aufanye,” amesema.

Aidha, Rais Magufulin amezitaka Asasi za Kiraia zinazopigania suala la wanafunzi kuruhusiwa kusoma baada ya kujifungua zifungue shule za wazazi badala ya kuilazimisha serikali kusomesha wazazi na kwamba serikali ipo tayari kuruhusu shule hizo zisajiliwe.

“Hata kama amezaa kwa bahati mbaya, yapo mambo mengi ya kufanya ukiwa mjamzito, kuna njia mbadala za kujiendeleza kama kwenda katika chuo cha mafunzo ya ufundi – VETA, anaweza akajifunza cherehani au akafanya kilimo cha kisasa,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!