July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli awatangazia kiama watendaji wabovu

Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli akihutubia wananchi Zakheem, Mbagara jijini Dar es Salaam

Spread the love

JOHN Pombe Magufuli, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania hatomuogopa mtu yeyote ambaye ataenda kinyume na utaratibu uliopagwa na serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana nchini. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

“Ninataka niseme kwa dhati kutoka moyoni. Sitamuogopa mtu na wala sitopenda mtu wa chini aonewe. Mimi sio mkali.Ni mpole kweli. Ila nawachukia sana watendaji wa serikali wabovu. Nazungumza jua linawaka. Akiamungu nitalala nao mbele,” amesema Dk. Magufuli.

Dk.Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi, ametoa kauli hiyo leo katika viwanja vya Mbagala Zakhiemu jijini Dar es Salaam, wakati yeye na Samia Suluhu, mgombea mwenza ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano, wakijitambulisha kwa wananchi na kuwashukuru wanachama wa CCM kuwapitisha ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Hatua ya CCM kuufanyia mkutano huo katika eneo la Mbagala inakuja, baada ya kubaini kuwa eneo hilo ni ngome ya Chama cha Wananchi CUF, hivyo hatua hiyo itasaidia CCM kujiimarisha katika eneo hilo.

Amesema ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana, atahakikisha anaongoza kwa kutekeleza Ilani ya CCM ambayo inasimamia masuala mbalimbali ikiwemo haki, barabara, afya, kilimo, biashara, reli na maji huku akisisitiza kuondoa kero zinazowakabili wafanyabiashara ndogondogo na madereva wa bodaboda.

“ Mwanachama wa Chadema, CCM, UDP na asiye na chama wote wanahitaji maendeleo. Sipendi nifafanue yote, ili watu wengine wasije kusema nilianza kampeni mapema. Nimekuja kujitambulisha. Jina langu ni John Pombe Joseph Magufuli, amesema Magufuli.

Kwa upande wake Samia amesema kwa ufupi kuwa, ushindi wa CCM utatokana na umoja utakaojegwa na wanachama wa chama hicho na wale ambao sio wanachama.

Awali kabla ya Magufuli kuzungumza, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM amesema, “Rais amesema yeye alikuwa mpole, sasa tumepata mtu mkali na juzi alisema atawashughulikia watu wote wanaokwenda kinyume na utaratibu.”

Mkutano huo ambao ulihudhuliwa na Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Said Meck Sadiki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na wabunge kadhaa wa chama hicho ulianza saa 8.45 mchana mara tu msafara wa Magufuli ulipowasili.

Msafara huo ulianzia katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na kusindikizwa na msururu wa magari na makundi ya bodaboda huku Nnauye akiingia katika viwanja hivyo akiwa amepakizwa nyuma ya moja ya bodaboda hizo.

Pia viwanja hivyo vilivyofurika mamia ya wafuasi wa CCM, huku kukiwa na mabasi zaidi ya 70 kutoka kampuni ya usafiri ya Dar es Salaam ( UDA) na watu binafsi ambayo yametumika kuwaleta wanachama hao kutoka katika maeneo mbalimbali ya jiji.

error: Content is protected !!