RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefuta maboresho yaliyotangazwa na wizara ya elimu nchini humo ya mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kufutwa na kutangazwa mpya wa Diploma ya awali na msingi kuanzia mwaka 2020/21. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Amesema, Serikali anayoingoza ilianza na walimu wa ngazi zote na itamaliza nao huku akiwataka waipuuze “tangazo hilo ni la kipumbavu limetolewa na wabaya wetu.”
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 5 Oktoba 2020 alipopiga simu kwenye kongamano la Walimu lililofanyika jijini Dodoma.
Kongamano hilo linafanyika siku ya walimu duniani ambapo Rais Magufuli amepiga simu kuwasalimia wakati mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akizungumza.
Mara baada ya kupiga simu, Rais Magufuli alimweleza Waziri Mhagama ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusogeza simu katika kipaza sauti ‘mic’ ili azungumze na walimu hao ambao wakati huo walikuwa wakimshangilia.
“Walimu hamjambo,” Rais Magufuli ambaye amewahi kuwa mwalimu amewasalimua walimu ambao wameitikia, hatujamboooooooo
“Leo ni siku yetu sisi walimu, nawapongeza sana kwa siku ya leo, wakati tunakumbuka siku ya walimu duniani na nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Waziri (Mhagama) ambaye ametumwa na Waziri Mkuu ambaye ni mwalimu na mimi ni mwalimu.”
Huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema “nataka kuwathibitishia tuko pamoja na ninyi, kuna tangazo moja linazunguka zunguka sijui linasema walimu wa cheti sijui wa nini mlipuuze tangazo hilo ni tangazo la kipumbavu.”
“Sisi tulianza na ninyi walimu, tutamaliza na ninyi walimu na ni walimu wote kuanzia wa cheti mpaka wa juu hata mke wangu (Janeth) ni mwalimu wa cheti, hata mke wa mwalimu Majaliwa (Mary) ni mwalimu.”
“Kwa hiyo walimu wa cheti tunawathamini kama walimu wengine, muipuuze hiyo taarifa najua imetolewa na wabaya wetu. Chapeni kazi,” amesema Rais Magufuli.

Ameendelea kusema “nafahamu kazi kubwa mnayoifanya na ndiyo maana tumetangaza nafasi zingine za 13,000 ili kupunguza tatizo hili.”
“Mimi nafahamu machungu ya walimu, nafahamu shida za walimu na nafahamu walimu wanataka nini. Walimu hongereni na Mungu awabariki sana,” amesema
Rais Magufuli, amewataka kutumia kongamano hilo kujadili kwa uwazi na kuzungumza kama walimu “tunavyojua kuzungumza. Nawapenda sana.”
Mapema leo Jumatatu asubuhi akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Ave Maria Semakafu alitangaza uamuzi wa Serikali kupitia wizara hiyo kuhusu maboresho ya mtaala wa ualimu ngazi ya Diploma uliokuwa uanze mwaka wa masomo 2020/21.
Alisema, mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi umefutwa na kuanzia mwaka 2020/21 utaanza kutolewa kuanzisha wa Diploma ikwa ni hatua ya kuboresha elimu nchini humo.
Mtaala huo ulioboreshwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, ulikuwa uwezeshe wanaojiunga na mafunzo ya ulimu kusoma kwa miaka mitatu.
Dk. Semakafu alisema, ulioboreshwa unatoa nafasi kwa mwalimu katika mwaka wa pili wa masomo kuchagua eneo la umahiri atakalobobea tofauti na mfumo wa zamani ambao haukuwa katika muktadha huo.
Alisema, walimu walioko tayari vyuoni wakisoma cheti ambao watamaliza mwaka 2021 hao ndiyo wangekuwa wa mwisho kudahiliwa hali ambayo haitakuwa hivyo kutokana na agizo la Rais Magufuli.
“Mtaala huu mpya utaanza kutumika mwaka wa masomo 2020/21 na mwalimu yeyote mwenye cheti cha ualimu atakuwa na sifa ya kusomea Diploma ya ualimu wa elimu ya awali au msingi na vilevile atakapohitimu na kufaulu atakuwa na sifa ya kujiunga na Chuo Kikuu kupata shahada ya kwanza ya ualimu wa elimu ya awali au msingi,” alisema Dk. Semakafu
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania , Aneth Komba alisema, “tumeboresha na kuongeza hadhi ya ualimu. Sasa tutakuwa na Diploma na zamani mtakumbuka tulikuwa hatuna shahada ya shule za msingi, lakini tunakwenda kuianzisha.”
“Tunataka kuwafanya kuwa wabobezi na tutaongeza walimu bora zaidi kwa walimu wenye cheti waliopo kazini, tumeandaa programu rafiki ya masafa na watasoma wakiwa kazini na kipindi cha likizo wataweza kukutana vyuoni kwa ajili ya kufanya mitihani,” amesema Aneth
Leave a comment