July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atonesha ‘donda’ la Mbowe

Spread the love

RAIS John Magufuli amepongeza hatua ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kumwondoa Freeman Mbowe, katika jengo ambalo amekuwa akipanga kwa muda mrefu, anaandika Pendo Omary.

Siku tano zilizopita, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia Mbunge wa Jimbo la Hai aliondolewa kwenye jengo hilo na mawakala wa NCH, Fosters Auctioneers kwa madai ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 1.3 Bilioni huku mvutano wa kuwepo kwa uhalali wa deni hilo ukiendelea.

Jengo hilo lipo katika makutano ya Mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam ambapo mawakala hao walichukua vifaa vya kampuni hiyo katika upande wa uzalishaji Gazeti Tanzania Daima chini ya Kampuni ya Free Media.

Rais Magufuli alilisifu shirika hilo leo asubuhi wakati akizungumza na baadhi ya waliokuwa wapangaji katika nyumba za NHC zilizokuwepo Magomeni Kota ambazo zilibomolewa mwaka 2012.

Kwenye mkutano huo Rais Magufuli amelitaka shirika hilo ndani ya siku saba kuwaondoa wapangaji wote wanaodaiwa na serikali kwenye nyumba zake.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amesema, ndani ya miezi miwili kuanzia leo serikali itaanza kujenga nyumba za waliokuwa wakazi wa eneo hilo.

Waliokuwa wapangaji katika nyumba za Magomeni Kota zilizomilikiwa na serikali waliondolewa kwa mkataba na Manispaa ya Kinondoni katika makazi hayo mwaka 2012 kupisha ujenzi wa makazi mapya kwa muda wa mwaka mmoja.

Katika mkataba huo makubaliano yalikuwa; manispaa hiyo kuwalipa wapangaji hao kodi ya nyumba ya muda wa mwaka mmojo na mara baaya ya ujenzi kupangishwa katika nyumba hizo na baadaye kuuziwa, hata hivyo mpaka sasa hakuna kilichotekelezwa.

Rais Magufuli amesema, “kwa sasa eneo hili la heka 33 lipo mikononi mwangu. Ndani ya miezi miwili, tutaanza kujenga nyumba na majengo ya mwanzo ni ya wakazi 644. Tutaanza kutoa fedha mwezi huu.

“Yatakapo malizika kujengwa, orodha ya majina yote ninayo wawe wapo hai au watoto wao ndio watakaoingia kwenye nyumba hizo. Nikishamaliza kujenga hizo nyumba hao wakazi 644 watauziwa nyumba.”

Rais Magufuli amesema, ujenzi wa nyumba hizo utakapokamilika ndani ya muda wa mwaka mmoja kuanzia sasa, kabala ya wakazi hao kuuziwa nyumba hizo, serikali itawaruhusu kuishi kwa muda wa miaka mitano bila kulipa kodi ambapo baada ya muda huo kupita ndipo watauziwa. Hatua hiyo inalenga kufidia ghalama walizotumia tangu waondolewe katika nyumba hizo.

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!