December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atokwa machozi akimwelezea Mkapa

Rais John Magufuli akishindwa kujiuza machozi kumtoa

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amejikuta akitokwa machozi hadharani baada ya shindwa kujizuia wakati akielezea mazungumzo yake ya mwisho na Rais mstaafu awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hilo limejitokeza leo Jumanne tarehe 28 Julai 2020 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kulipokuwa kunafanyika shughuli ya kuaga Kitaifa mwili wa Mkapa aliyefariki dunia Alhamisi tarehe 23 Julai 2020 saa 3:30 usiku kwa mshituko wa moyo.

Akihutubia taifa katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji uwanjani hapo, Rais Magufuli amesema “hakuna mtu anayeweza kumwelezea vizuri Mzee Mkapa zaidi alivyojieleza mwenyewe vizuri kwenye kitabu chake cha My Life, My Purpose.” (Maisha Yangu, Kusudio Langu).

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ambaye alikuwa mara kadhaa anatulia, akilengwa lengwa na machozi akisema kifo cha Mkapa ni pigo kwani ilizoeleka katika matukio makubwa anaungana na marais wenzake wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Mrisho Kikwete ‘lakini leo hapa hayupo.”

         Soma zaidi:-

“Mzee Mkapa alinilea kama mtoto wake, alikuwa ni shujaa wangu, alinionyesha upendo,

“Hata kwenye shida Mzee Mkapa hakuniacha kamwe, hakutaka nianguke, alinilea kama mtoto wake. Wakati wote alikuwa ananionyesha upendo, hivyo basi kuondoka kwake ni pigo kubwa kwangu, nimepoteza mtu muhimu kwangu.”

“Saa nyingine machozi yanakuja tu msinishangae sana, hata Mzee Kikwete nilimuona juzi anadondosha machozi tena Kikwete ni Kanali ila alitoa chozi kwahiyo msinishangae mimi,” amesema Rais Magufuli

“Nilipata fursa ya kuongea na Mzee Mkapa kwa simu akiwa hospitalini saa chache kabla hajafariki, nakumbuka aliniambia John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri sikujua kwamba maneno yale yalikuwa ya kuniaga. kazi ameikamilisha,” amesema Rais Magufuli huku akitulia na kutoa kitambaa kufuta machozi.

Rais Magufuli amesema “Mzee Mkapa alikuwa na vipaji vya kulea na kukuza, yeye ndiye aliniibua mimi, alimteua Mzee Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 baadaye akawa mrithi wake.”

“Yeye alimuibua Rais wa sasa wa Zanzibar Dk. (Ali Mohamed) Shein, kufuatia kifo cha Makamu wa Rais Hayati Omari Ally Juma na alimuibua Dk. Hussein Mwinyi kama mnavyofahamu hivi sasa ni mgombea urais Zanzibar, hii inadhihirisha Mzee Mkapa alikuwa na uono wa kuona viongozi.”

Amesema, Mzee Mkapa alimuibua Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye kwa sasa ni Mgombea Urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa mwandishi wake wa hotuba Balozi Ombeni Sefue baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Rais John Magufuli akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Hayati Benjamin Mkapa

Shughuli hiyo imemalizika kwa Rais Magufuli kuondoka uwanjani hapo na baadaye mwili huo utasafirishwa kwenda Kijijini kwake, Lupaso, wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara kwa maziko yatakayofanyika kesho Jumatano tarehe 29 Julai 2020.

error: Content is protected !!