August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atoboa udhaifu wa polisi

Spread the love

RAIS John Magufuli leo ameeleza udhaifu wa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na ujambazi nchini, anaandika Regina Mkonde.

Mkuu huyo wa nchi ameonesha kushangazwa na majambazi kutamba wakati Jeshi la Polisi lina silaha za kutosha, hivyo kuhoji kulikoni?

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akihutubia katika uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Jamii uliofanyika katika viwanja vya Biafra, jijini Dar es Salaam.

“Kuna baadhi ya mambo yananikera, jambazi anakuja anaiba na kuondoka haraka wakati Jeshi la Polisi lina bunduki nyingi zenye risasi,” amesema na kuongeza;

“Kama amekuja na bunduki, ina maana hajaja kufanya maonesho bali amekuja kufanya kazi. Mkimuona jambazi mnyang’anye bunduki haraka na atakaye mnyang’anya asipelekwe mahakami apandishwe cheo, mkifanya hivi mtanifurahisha.”

Rais Magufuli amelitaka jeshi hilo kutumia mbinu zinazopendwa kutumiwa na majambazi katika kukabiliana nao.

“Watu wanapokonywa mali zao kwa njia ya bodaboda, na nyie askari polisi tumieni bodaboda wakati mnapopambana,” amesema.

Rais Magufuli ametoa wito kwa viongozi wa Jeshi la Polisi kutowabana polisi wadogo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa madai huchelewesha kufanya kazi zao.

“Vijana wenu wanaweza kuwa na moyo wa kufanya kazi lakini inawezekana mnawabana   na kuwachelewesha kufanya kazi. Mkisimama imara wapo vijana wengi wenye moyo wa kufanya kazi,” amesema.

Pia amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwapa posho maalum polisi ambao watakuwa na kazi ya kupokea simu za wahalifu na pia kuwachagua polisi wenye maadili.

“Wale vijana wapo wanaofanya kazi kwa shifti, waangaliwe namna ya kupewa posho maalum,” amesema.

Kuhusu mpango uliozinduliwa leo Rais Magufuli amelitaka jeshi hilo kuchagua polisi waadilifu ambao watafanya kazi ya kupokea taarifa za wahalifu.

“Pamoja na mpango kuwa mzuri, inawezekana mtu mwema akapiga simu halafu wasiokuwa waaminifu wakamwambia jambazi hatimaye mtoa taarifa akashughulikiwa,”amesema.

Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kuwa, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la kutoto stakabadhi baada ya kumhudumia mteja, atahukumiwa pasipo kufanyika kwa upelelezi.

“Wananchi tunahitaji ushirikiano wenu wa kutoa taarifa za uhalifu ukiwemo ujambazi, pamoja na ukienda dukani mwenye duka akikwambia akupe risiti ya duka au ya TRA toka nje, piga simu na kwamba itajulikana eneo ulipo na gari la polisi lililopo eneo hilo litapewa taarifa na kuja katika eneo la tukio,” amesema.

Amesema, suala hilo halina upelelezi hususan kwa wale waliokamatwa na bidhaa kwa kuwa, wengi wao hukwepa kutoa risiti kutokana na kutokuwa na bidhaa halali sokoni.

“Kwa wale wanaotetea wahalifu wajiandae kisaikolojia, hakuna mhalifu atakayeachwa hata akifanyia nyumbani kwake,” amesema.

error: Content is protected !!