RAIS wa Tanzania, John Magufuli amemteua Profesa Shukrani Manya kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Brightnes Boaz, Dar es Salaam … (endelea).
Pia, Profesa Manya ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema, Profesa Manya ataapishwa leo Ijumaa mchana tarehe 11 Desemba 2020, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Kabla ya kiapo hicho cha uwaziri, saa 5:00 asubuhi ya leo, Spika wa Bunge, Job Ndugai atamwapisha kuwa Mbunge.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Manya alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania.
Profesa Manya, ameteuliwa kujaza nafasi ambayo Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane alishindwa kuapa vizuri, kiapo cha naibu waziri.
Tukio hilo lilitokea Jumatano ya tarehe 9 Desemba 2020, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo, Rais Magufuli aliwaapisha mawaziri 21 na naibu wao 22.
Rais Magufuli alisema, atafanya uteuzi wa naibu waziri mwingine wa madini ambaye ataweza kusoma vizuri nyaraka na Ndulane atasalia na nafasi yake ya ubunge.
Leave a comment