August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atangaza vita na magazeti

John Magufuli, Rais wa Tanzania alipokuwa kwenye ziara mkoani Shinyanga

Spread the love

RAIS John Magufuli amesema kwamba utawala wake upo mbioni kuyachukulia hatua kali magazeti mawili hapa nchini kwa madai kuwa yamekuwa yakifanya uchochezi, anaandika Mwandishi wetu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Shinyanga, Rais Magufuli amesema mauaji ya watu milioni moja yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda, yalichochewa na vyombo vya habari hivyo serikali yake itachukua hatua kali dhidi ya magazeti mawili ambayo hakuyataja.

“Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi. Hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la kuweka maneno ya uchochezi, chini ya utawala wangu hilo halitakuwepo. Na ni magazeti mawili tu, kila ukisoma wao wanachochea tu,” amesema Magufuli huku akiongeza;

“Nasema na nataka wanisikie, siku zao zinahesabika. Kama wanasikia wasikie. Magazeti mengine na vyombo vingine vyote vinatoa uchamuzi mzuri bila kuchochea wala kuleta chokochoko. Sitakubali Tanzania ikose amani kwa sababu ya vyombo vya habari vichache vinavyotumiwa na wanasiasa.”

Kauli hii ya Rais Magufuli inakuja wakati ambao utawala wake unashutumiwa kwa ukandamizaji wa uhuru wa habari ikiwemo kutunga sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari na waandishi. Baraza la Habari hapa nchini (MCT), tayari limefungua kesi kupinga Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Magufuli pia magazeti mawili yamewekwa kitanzini ambapo gazeti la MAWIO limefutiwa usajili huku gazeti la MSETO likifungiwa kwa miaka mitatu – kuanzia Agosti 2016 mpaka Agosti 2019.

Ndani ya mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli pia vituo viwili vya redio vimefungiwa kwa muda kabla ya kuachiwa huku vikipewa onyo kali kwa tuhuma za uchochezi. Vituo hivyo ni redio 5 na Magic FM.

error: Content is protected !!