July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atangaza siku tatu za maombi

Rais John Magufuli

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, ametangaza siku tatu za maombi kuanzia leo Ijumaa hadi Jumapili tarehe 21 Februari 2021, ili Mungu atokomeze tatizo la changamoto za upumuaji. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametoa wito huo leo tarehe 19 Februari 2021, katika ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Balozi Kijazi (64), alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021, Hosputali ya Benjamin Mkapa, alipokuwa amelazwa na mwisho wake, utazikwa kesho Alhamis, Korogwe jijini Tanga.

Rais Magufuli amewaomba waumini wa dini ya Kiislamu, kuitumia Ijumaa ya leo kufanya maombi hayo sambamba na kufunga, huku akiwahimiza Wasabato kufanya maombi hayo kesho Jumamosi, na wakristo wengine Jumapili.

“Waislamu walitanagza muda wao wa kuomba, niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tuliteteleka tumuombe Mungu. Tuanze leo kwa Waislamu, kesho Jumamosi kwa ndugu zetu Wasabato na Jumapili kwa Wakristo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza “kwa siku tatu kwa kuomba na kufunga, nina hakika tutashinda, tutahangaika sana Mungu ni mwenye uwezo wa kila kitu.”

Rais Magufuli amewaomba viongozi wa dini nchini, kuendelea kuwahamasisha waumini wao kufanya maombi hayo, ili Taifa lishinde kama lilivyoshinda katika maombi dhidi ya janga la mlipuko wa virusi vya corona mwaka 2020.

“Niwaombe viongozi wa dini kama mlivyokuwa mkifanya endeleeni kutangaza maombi tutashinda, tulishinda mwaka jana, mwaka huu mpaka tukaingia uchumi wa kati na corona ipo.

“Uchumi ukaendelea kupanda corona ipo, miradi ikaendelea kutekelezwa wala hatukuweka lockdown (karantini) miradi ikaendelea kutelezwa na corona ipo, hata sasa hatutaweka lockdown sababu Mungu yupo,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametangaza siku hizo za maombi akisema, kuna baadhi ya Watanzania wameanza kutisha wenzao hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kupoteza imani yao juu ya uwezo wa Mungu.

“Ninachotaka kusema ndugu zangu Watanzania, magonjwa yapo, yataendelea kuwepo. Magonjwa ya kifua, ya kupumua yatakuwepo, na hayakuanzia hapa, ziko nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi sisi Watanzania Mungu ametusaidia katika kipindi cha mwaka uliopita,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza “tulishinda mwaka jana, inawezekana hili ni jaribu lingine, tukisimama na Mungu tutashinda. Tusitishane na kuogopeshana tutashindwa kufika, inawezekana kuna mahali tumekosea Mungu, kuna mahali tunapata jaribu kama Waisrael kwenda Kanani tusimame na Mungu, kufa tutakufa tu unaweza ukafa kwa malaria.”

Rais Magufuli amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya changamoto ya upumuaji.

“Tuendelee kusimama kwa kuchukua tahadhari lakini pia kumtanguliza Mungu, imefikia mahali hapa njiani watu wananza kusita hata nguvu za Mungu, tumeanza kutegemea nguvu za binadamu. Narudia kuwaomba wenzangu tujue Mungu yupo ndio muweza wa yote,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!