May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli atamuweza Lowassa mahakamani?

John Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

NIMEPATA mrejesho kutoka kwa wasomaji wa safu hii kutokana na uchambuzi wa wiki iliyopita, uliofananisha wongofu wa ghafla wa Sauli na mabadiliko ya ghafla ya Lowassa. Miongoni mwa watu 206 waliowasiliana nami kwa njia mbalimbali, wapo watatu ambao hawakupendezwa na kazi yangu, anaandika Ansbert Ngurumo.

Wengine 203 walikubaliana nami; na baadhi yao walihoji kwanini sikuandika uchambuzi huu wakati wa kampeni za mwaka jana. Nilijibu baadhi yao, na kunyamazia wengine.

Kwa kuwa niliahidi kuendelea na uchambuzi huu leo, nimelazimika kuchukua moja ya maswali niliyotupiwa, ili kukamilisha uchambuzi huo.

Msomaji mwenye namba ya simu +255714908575 aliandika hivi: “Kupitia makala yako, ‘Lipumba wa jana si bora kuliko Lowassa wa leo’ tafadhali naomba ujibu swali hili: Lowassa alihamia Chadema akitokea CCM baada ya kukatwa jina lake.

“Uhalali wa kupigania wanyonge anaupata wapi? Je, kama asingekatwa jina kule CCM, angekuwa mpigania wanyonge? Kama Lowassa kweli alijiuzulu uwaziri mkuu na akijua kuwa kweli hakuwa mhusika wa Richmond, kwanini alikubali kufanya hivyo?”

Haya ni maswali matatu. Nitayajibu kwa kifupi. Lakini kabla sijayajibu, ningependa wasomaji waelewe kwamba sitaendelea kujibu maswali yamhusuyo Lowassa, kwa sababu kwanza si kazi yangu kujibu maswali yake, lakini pia mimi si msemaji wake.

Kilichotokea ni kwamba nimekuwa naulizwa maswali juu yake kwa kuwa huko nyuma, niliwahi “kumsema” akiwa waziri mkuu. Kwa hiyo, wapo wanaoshangazwa kwanini sasa badala ya “kumsema” namzungumzia vizuri. Nilijibu swali hili kwa kirefu Jumatatu iliyopita, kwamba Lowassa wa CCM si Lowassa wa Chadema.

Nilisisitiza pia kwamba Profesa Ibrahim Lipumba wa jana si wa leo, na kwamba Yuda aliyeishi na Yesu kwa miaka mitatu akishika mikoba ya kundi la mitume, alipoteza wema wote siku alipomsaliti kiongozi wake; na kwamba Sauli aliyekuwa anatesa wakristo, alisamehewa tangu siku alipojiunga na wakristo baada ya pigo alilopata akiwa njiani kwenda kuumiza wakristo.

Kwa hiyo, kwamba Lowassa alikatwa jina lake akiwa CCM ndipo akahamia Chadema, si jambo gumu kuelewa, kwani hiyo ndiyo ilikuwa njia yake ya kujiunga na wapambanaji dhidi ya CCM. Ilibidi akatwe ili shabaha nyingine itimizwe.

Na hapa ndipo panapopatikana jibu la swali la kwanza la msomaji wetu. Lowassa asingepata uhalali wa kupigania wanyonge akiwa ndani ya mfumo ule ule uliowafanya wananchi wawe wanyonge. Yawezekana Mungu alitaka akae huko kwa wanyanyasaji, ashiriki dhambi zao, aumize wanyonge; ili wakati utakapofika aweze kujua kiwango cha nguvu, akili, na raslimali nyingine anazopaswa kutumia kuwatetea.

Ni sawa na shehe aliyeongokea Ukristo. Akipata jukwaa la kutetea ukristo dhidi ya imani yake ya zamani, huwa mkali kuliko mchungaji aliyezaliwa katika familia ya Kikristo, kwa sababu anajua siri ya ndugu zake wa zamani. Vile vile kwa padre aliyeasi ukristo akageukia uislamu. Anaweza kuwa mhubiri mzuri kwa waislamu kuliko Muislamu aliyezaliwa na kusilimishwa akiwa mtoto.

Mang’amuzi na uzoefu wake ni nyenzo za harakati zake mpya katika kueneza imani mpya aliyoongokea ukubwani. Kwa hiyo,  Lowassa anapata uhalali wa kupigania wanyonge kwa sababu mbili.

Kwanza, amepata fursa ya kuona ubaya wa kile alichokuwa anatetea miaka yote akiwa mwanaCCM. Dhamiri yake inamsuta kwamba alichelewa kuelewa hoja ya wapinzani, aliwaamini sana wenzake katika CCM, lakini wao walimtumia na kumtema kama ganda la muwa.

Nahisi atakuwa anajiuliza: “Kama walifanya haya dhidi yangu, itakuwaje kwa hawa walio wadogo na wanyonge zaidi?” Hizi ni hisia binafsi zinazomsadia kutafsiri maumivu ya wananchi wengine. Akiwa mwanasiasa anayetamani uongozi, angependa kutoa mchango kwa kutumia uwezo na fursa alizonazo kusemea na kutetea wanyonge.

Pili, anapata uhalali kutoka kwenye taasisi mpya aliyojiunga nayo. Na hapa ndipo ulipo umuhimu wa uamuzi wake. Kama Lowassa angekatwa, halafu akabaki ndani ya CCM, huku yeye na wenzake wakilalamika na kunung’unika, asingekuwa tofauti na Samwel Sitta ambaye mara mbili CCM imemdhalilisha baada ya kumtumia.

Mara ya kwanza ni mwaka 2010 alipotaka kugombea uspika, chama chake kikaweka sharti gumu sana la kijinsia, kwamba anahitajika spika mwanamke. Pale pale, Sitta alijua kuwa hatakiwi. Alidiriki kuhama chama, akaomba kujiunga na Chadema, lakini nguvu za dola zikamzuia, na viongozi wa Chadema wakamkataa, kwa kuwa alikuwa ameshawasaliti miezi michache kabla.

Mara ya pili CCM ilimhujumu Sitta mwaka 2015 alipotaka urais, lakini akaondolewa kwenye kinyang’anyiro bila hata kusikilizwa, akajumuishwa na akina Lowassa.

Tukio hili lilimstua Lowassa, likamduwaza Sitta. Ghafla, baada ya kuhamia Chadema, Lowassa akawa shujaa miongoni mwa wananchi wale wale waliowahi kumshambulia. Kilichowafurahisha wengi ni kwamba Lowassa alitambua umuhimu wa kupigana dhidi ya CCM, badala ya kupigania CCM.

Kama muumini mpya katika imani mpya, Lowassa akalazimisha kujifunza na kushiriki mapambano ya kuondoa CCM. Akawa adui wa watawala. Na kwa sababu hiyo, akawa rafiki na mtetezi wa wanyonge.

Hii ndiyo sababu iliyokuza heshima yake na kushusha ya akina Sitta na Joseph Warioba, ambao huko  walijaribu kupambana na serikali, wakaungwa mkono na wanyonge; lakini wakati muhimu wa uamuzi ulipowadia Sitta na Warioba wakajiunga na serikali na kupambana na wanyonge.

Warioba akasahau kuwa CCM aliyokuwa anainadi majukwaani, isingekubaliana kabisa na rasimu yake, isingeleta katiba mpya; na kwamba Lowassa aliyekuwa anashambuliwa na akina Warioba tayari alikuwa amejiunga na wanyonge wanaotaka kurejesha na kutetea rasimu ya Warioba kwa ajili ya kupata katiba mpya itokanayo na maoni ya wananchi.

Je, kama asingekatwa jina akiwa CCM angeweza kuwa mtetezi wa wanyonge? Hapana! Huwezi kuwa mtetezi wa wanyonge ukiwa upande wa watawala, wanaonyanyasa na kuhujumu wanyonge.

Huwezi kuwa mtetezi wa wanyonge ukiwa mtetezi wa sera na mipango inayonyonya wanyonge. Huwezi kuwa mtetezi wa wanyonge ukiwa sehemu ya utawala ule ule unaoumiza wanyonge. Kwamba aliamua kuondokana na mfumo huo, ni sifa ambayo hakuna mtu anayeweza kumnyang’anya.

Na hapa alikuwa anajibu swali hilo la tatu kuhusu Ricmond. Lowassa hajawahi kumiliki Richmond. Lakini amewahi kuitetea ipate mradi wa kuzalisha umeme. Vile vile, akiwa waziri mkuu, Lowassa amewahi kutaka serikali ivunje mkataba na Richmond, rais akagoma.

Ndiyo maana alipohamia Chadema, aliwaambia wenye shaka naye kuhusu sakata la Richmond, aliwataka wampeleke mahakamani. Hadi leo hawajamfikisha mahakamani. Na wapo wanaodhani kwamba kwa kuundwa mahakama ya mafisadi, Lowassa wa Richmond atakuwa wa kwanza kushitakiwa; ili nione nani atashinda kesi hiyo. Naisubiri kwa hamu siku hiyo.

Makala hii imetoka kwenye Gazeti la MwanaHALISI la tarehe 10-16 Oktoba, 2016

 

 

error: Content is protected !!