June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli asitisha bomoabomoa

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza kutobomoa nyumba zilizopo kando kando ya barabara ya Mwanga-Kikweni/Vuchama-hadi Lomwe yenye urefu wa kilomita 40.6. Anaandika Mwandishi wetu… (endelea).

Badala yake Dk. Magufuli anasema kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia upana wake uliopo sasa hivi.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo ya “faraja” kwa wakazi wa Kikweni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kabla ya kuweka jiwe la msingi katika barabara hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni.

Waziri amechukua uamuzi huo kutokana na maeneo mengi ya milimani ambapo barabara hiyo inapita kuwa na mashamba ya watu tofauti na sehemu nyingine.

“Nikiwa kama waziri wa ujenzi katika maeneo haya ya milima sitatumia sheria ya mita 30 kila upande katika ujenzi wa barabara hii ili nyumba na mashamba ya wakazi wa huku yasiathirike,” anaesema.

Dk. Magufuli ameongeza kuwa ujenzi wa barabara una sheria zake- ndio maana ameamua kutumia sheria ya barabara namba 13 ya mwaka 2007 kifungu cha 13 na 20 kinachompa mamlaka kupunguza upana wa barabara.

Aidha, Dk. Magufuli amewatoa hofu wakazi wote waliowekewa alama ya X katika nyumba zao na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa sababu nyumba hizo hazitabomolewa.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli amewataka watu wote waliojenga vibanda karibu na barabara ya zamani waanze kuondoka mapema kabla ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza hivi karibuni.

“Nawaomba wote mlioweka vibanda karibu na barabara mtoe kwa hiari yenu ili tutengeneze barabara hii bila vikwazo na kwa haraka tofauti na awali ambapo tulikuwa tunatangaza zabuni kwa kilomita chache,” amesema.

Kwa upande, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amemshukuru Waziri Magufuli kwa hatua yake hiyo na kusema kuwa kufunguka kwa barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wilaya ya Mwanga na mkoa mzima kwa ujumla.

Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe ameishukuru Serikali na kusema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawaondolea kero kubwa ya usafiri wananchi wa Usangi na Mwanga -na kuwasaidia kufanya biashara kwa urahisi zaidi tofauti na awali.

error: Content is protected !!