December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli asimulia alivyonusurika kifo, atua Chato

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, lililopo jijini Mwanza, litakalokuwa na urefu wa 3.2 kilometa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Daraja hilo ambalo linajengwa na mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kwa gharama ya takribani Sh.700 bilioni, linatarajiwa kukamilika Februari mwaka 2024.

Rais Magufuli alifanya ukaguzi wa daraja hilo jana Jumatatu, tarehe 28 Desemba 2020, akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda kijijini kwake, Chato mkoani Geita.

Akizungumza mbele ya Rais Magufuli, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Mwanza (TANROADS), Mhandisi Vedastus Maribe, ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulioanza tarehe 25 Februari 2020, umefikia asilimia 11.18, ikiwemo ujenzi wa daraja la muda ambao umefikia 51.6 asilimia.

Alisema, daraja hilo lilikamilika,  linatarajiwa kuwa na nguzo 67 zikiwemo tatu kubwa.

Akizungumza baada ya kujionea kazi ya uchimbaji wa mashimo yenye urefu wa meta tatu ndani ya mwamba kwa ajili ya ujenzi wa nguzo hizo, Rais Magufuli alisema, amefurahishwa na hatua iliyofikiwa.

Hata hivyo, amemtaka mkandarasi anayejenga jingo hilo, kuongeza kasi ya ujenzi ikiwamo kufanya kazi usiku na mchana, ili mradi huo uweze kukamilika haraka.

“…daraja hili lina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Tanzania na nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na DRC,” ameeleza Rais Magufuli.

Rais Magufuli alitumia fursa hiyo, kusimulia mkasa uliosababisha kuamua kujenga daraja hilo, kwamba ni kutokana na alivyonusurika kufa maji baada ya mtumbwi aliokataa kuupanda kuzama na kusababisha vifo vya watu 11 waliopanda mtumbwi huo, uliotoka Busisi kwenda Kigongo.

Amesema, kujengwa kwa daraja hilo kutaepusha ajali za mara kwa mara za kuzama kwa mitumbwi inayovusha watu na bidhaa mbalimbali.

Ametoa wito kwa wananchi hasa vijana wanaopata ajira katika mradi huo, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuiba vifaa vya ujenzi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewapongeza wananchi kwa kuchapakazi na kulipa kodi ambayo ndio inayotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja hilo.

Ametoa wito kwa kila mwananchi kuhakikisha analipa kodi ipasavyo na kudai risiti kila anapofanya manunuzi ya bidhaa zake.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote kutumia mvua zinazonyesha nchini kote, kulima kwa wingi mazao mbalimbali hasa ya chakula, kwa kuwa mazao hayo yatahitajika katika nchi mbalimbali ambazo wananchi wake wamefungiwa (lockdown) kutokana na ugonjwa wa Korona (Covid -19) na hivyo kushinda kuzalisha mali ikiwemo kuzalishaji chakula kwa ajili ya mahitaji yao.

error: Content is protected !!